• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2018

    KARIA, KIDAU WAKOSEKANA OFISINI WAMBURA AKIKABIDHI BARUA YA KUREJESHWA MADARAKANI NA MAHAKAMA LEO ASUBUHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura leo amekabidhi barua ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutengua maamuzi ya Kamati za Maadili za shirikisho hilo kumfungia maisha kujihusishan na mchezo huo.
    Wambura amekabidhi barua hiyo asubuhi ya leo ofisi za TFF makao makuu, Uwanja wa Karume mjini Dar es Salaam na akasema atapeleka nakala Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). 
    Hata hivyo, Wambura hakufanikiwa kumkuta yeyote kati ya viongozi wakuu wa TFF, Rais, Wallace Karia au Katibu Mkuu, Wilfred Kidau hivyo barua hiyo akaikabidhi kwa maofisa wengine aliowakuta ambao walisiani kudhihirisha wameipokea.
    Michael Wambura akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisi za TFF, Uwanja wa Karume mjini Dar es Salaam 

    Na Wambura akasema baada ya kukabidhi barua huyo anarejea rasmi kazini katika wadhifa wake wa Makamu wa Rais wa TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM).
    “Sihitaji kuwaomba kurudi ofisini, mimi nilichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF, wao wakanifungia kujihusisha na soka. Nimekwenda mahakamani wametengua uamuzi wa mimi kufungiwa, hivyo nimerudi ofisini. Nimekuja hapa kuwafahamisha nimerudi na bado nipo,”amesema Wambura.
    Ijumaa Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, kupitia kwa Jaji, Dk. Benhajji Masoud ilitengua maamuzi ya Kamati za Maadili za TFF kumfungia Wambura maisha kujihusishan na soka kufuatia kesi aliyofungua kupinga maamuzi hayo.
    Kwa uamuzi huo, Wambura anarejea katika madaraka yake ya Umakamu wa Rais wa TFF na Uenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM).
    Maana yake, Athumani Nyamlani aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo sasa anapoteza wadhifa huo aliopewa baada ya kuwa Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji. 
    Katika kesi hiyo TFF, iliyo chini ya Rais Wallace Karia ilikuwa inawakilishwa Wakili David Ndosi, ambaye hata hivyo leo hakuonekana wakati wa hukumu. Nakala za hukumu zinatarajiwa kuwafikia TFF mapema Jumatatu.

    Walikuwa wapi? Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) na Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidau (kushoto) hawakuwepo ofisini leo wakati Wambura akikabidhi barua ya mahakama

     Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu.
    Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
    Ikumbukwe Wambura alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF Agosti 12, mwaka jana mjini Dodoma katika uchaguzi uliomuweka madarakani Karia katika nafasi ya Urais. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA, KIDAU WAKOSEKANA OFISINI WAMBURA AKIKABIDHI BARUA YA KUREJESHWA MADARAKANI NA MAHAKAMA LEO ASUBUHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top