• HABARI MPYA

    Monday, November 05, 2018

    SWEDI NKWABI BOSI MPYA SIMBA SC, VIONGOZI WALIOMALIZA MUDA WAO WOTE ‘WAFYEKELEWA MBALI’

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MFANYABIASHARA mdogo, Swedy Nkwabi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ukurugenzi ya Simba katika uchaguzi uliofanyika jana ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam.
    Swedi alikuwa mgombea pekee baada ya gwiji wa klabu, Mtemi Ramadhani kujitoa dakika za mwishoni na amepita bila kupingwa.
    Katika nafasi za Ujumbe, viongozi wote waliomaliza muda wao, Iddi Kajuna, Said Tuliy, Ally Suru na Jasmine Costa wameangushwa. 
    Waliochaguliwa katika nafasi za Ujumbe ni Hussein Kitta Mlinga, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Suleiman Haroub Said, Mwina Mohammed Kaduguda na Asha Ramadhani Baraka.
    Swedy Nkwabi ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Ukurugenzi ya klabu ya Simba 

    Wengine waliogombea nafasi za Ujumbe ni Mohamed Wandi, Abdallah Rashid Mgomba, Christopher Kabalika Mwansasu, Alfred Martin Elia, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakari Zebo na Patrick Paul Rweyemamu.
    Uchaguzi wa Simba SC umefuatia uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wake.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi huo.
    Nkwabi ambaye amekidhi matakwa ya Katiba mpya ya Simba SC kuwa na elimu ya Shahada sasa ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake huku akiwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SWEDI NKWABI BOSI MPYA SIMBA SC, VIONGOZI WALIOMALIZA MUDA WAO WOTE ‘WAFYEKELEWA MBALI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top