• HABARI MPYA

  Wednesday, November 07, 2018

  ALLIANCE WAIPIGA MTIBWA 1-0 NYAMAGANA, MWADUI FC WAITAFUNA LIPULI, NDANDA WAMELAMBWA NA COASTAL

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Alliance FC imeendelea kukunjua makucha baada ya leo kupata ushindi wake wa tatu wa msimu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia kuilaza 1-0 Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Shujaa wa Alliance FC leo amekuwa ni mshambuliaji wake mahiri, Dickson Ambundo aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 54.
  Kwa ushindi huo, Alliance FC inafikisha pointi 13 baada ya kuchezesha 14 ikipanda kwa nafasi tatu hadi ya 16, wakati Mtibwa Sugar inaendelea kushika nafasi ya nne kwa pointi zake 23 za mechi 14, ikiwa nyuma ya Azam FC pointi 30 mechi 12, Simba SC pointi 26 mechi 11 na Yanga SC pointi 26 mechi 10.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Jean- Marie Girukwishaka kwa penalti dakika ya 29, limetosha kuipa Mwadui FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Mwadui Complex wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
  Alliance FC leo wameshinda mechi ya tatu ya msimu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara 

  Na Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, bao pekee la Andrew Sinchimba dakika ya 12 limeipa ushindi wa 1-0 Coastal Union dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, huku Biashara United ikilazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
  Nayo Ruvu Shooting ikapoza machungu ya ‘vipigo vitakatifu’ 5-0 kutoka kwa Simba SC Dar es Salaam na 4-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar Morogoro kwa kuilaza 2-1 Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Mabao yote ya Ruvu Shooting leo yamefungwa na mshambuliaji wake Said Dilunga, kaka wa kiungo wa Simba SC, Hassan Dilunga dakika za 71 na 85 kwa penalti, baada ya Paul Materezi kutangulia kuifungia Stand United dakika ya 10.    
  Na Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, bao la dakika ya 90 la mkongwe, Nizar Khalfan likainusuru Stand United kupoteza tena mechi baada ya kupata sare ya 1-1 na wenyeji, Kagera Sugar waliotangulia kwa bao la Ramadhani Kapera kwa penalti dakika ya 33. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mchezo mmoja tu, Mbeya City wakiikaribisha JKT Tanzania Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALLIANCE WAIPIGA MTIBWA 1-0 NYAMAGANA, MWADUI FC WAITAFUNA LIPULI, NDANDA WAMELAMBWA NA COASTAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top