• HABARI MPYA

    Tuesday, October 16, 2018

    TAIFA STARS YAICHAPA CAPE VERDE 2-0 NA KUFUFUA MATUMAINI YA KWENDA CAMEROON 2019

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    TANZANIA imefufua matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Kundi L jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo wa kwanza kwenye mashindano haya, unaifanya Taifa Stars ijisogeze hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo usiku huu inamenyana na Lesotho mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake saba za mechi tatu, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
    Hadi mapumziko, Taifa Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lilillfungwa na kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Msuva dakika ya 29 akimalizia pasi nzuri ya Nahodha, Mbwana Samatta aliyemtoka beki wa kushoto wa Papa wa Bluu, Rodrigues Carlos. 
    Mbwana Samatta akishangilia baada ya kuifungia Taifa Stars bao la pili leo
    Mbwana Samatta akimtoka beki wa Cape Verde, Rodrigues Carlos
    Simon Msuva akitafuta maarifa ya kumpita beki wa Cape Verde, Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’
    Kiungo Mudathir Yahya akiwatoka wachezaji wa Cape Verde
    Mashabiki wakishangilia ushindi wa Taifa Stars leo Uwanja wa Taifa

    Awali, dakika ya 22 Nahodha Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aligongesha mwamba wa juu mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Michael Gasingwa wa Rwanda baada ya beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’ kumuangusha Msuva kwenye boksi.
    Msuva almanusra afunge tena dakika ya 38 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache kufuatia krosi ya Samata kutoka upande wa kushoto.
    Kipindi cha pili Taifa Stars walikianza kwa kais tena na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Nahodha, Samatta dakika ya 58 kwa shuti akimalizia pasi ya kiungo Mudathir Yahya Abbas.
    Baada ya bao hilo, kocha Mnigeria wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike alifanya mabadiliko katika safu ya kiungo, akimtoa Mudathir na kumuingiza Mzanzibari mwenzake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kabla ya kumtoa pia na beki Abdi Hassan Banda na kumuingiza John Bocco.
    Nahodha Mbwana Samatta ambaye ataukosa mchezo ujao dhidi ya Lesotho baada ya kuonyeshwa kadi ya njano ya pili, alimpumzishwa dakika za mwishoni baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa BDF ya Botswana, Rashid Mandawa. 
    Kikosi cha Taifa Stars kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Abdi Banda/John Bocco dk51, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathir Yahya/Feisal Salum dk58, Mbwana Samatta/Rashid Mandawa dk89 na Simon Msuva.
    Cape Verde: Graca Theirry, Almeid Tiago/Rocha Nuno dk64, Rodrigues Carlos, Barros Admilson, Tavares Ianique, Fortes Jeffry, Macedo Elvis, Rodrigues Garry, Soares Luis/Heldon Ramos dk53, Semed Jorge na Gomes Ricardo/Gilson Silva dk77. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAICHAPA CAPE VERDE 2-0 NA KUFUFUA MATUMAINI YA KWENDA CAMEROON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top