• HABARI MPYA

  Tuesday, October 16, 2018

  HANS POPPE AACHIWA KWA DHAMANA YA SH MILIONI 30 BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA 10 LEO KISUTU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameachiwa kwa dhamana baada ya kusomewa mashitaka 10 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam, Thomas Simba.
  Hans Poppe amewekewa dhamana ya Sh. Milioni 30 na watu wawili kwa kila mmoja kuweka Sh. Milioni 15 baada ya kuunganishwa kwenye kesi inayowakabili viongozi wengine wa Simba SC, Rais Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu'.
  Lakini Aveva na Kaburu wataendelea kusota rumande katika gereza la Keko mjini Dar es Salaam kwa sababu mashitaka yao hayana dhamana.
  Sasa Mjumbe huyo wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC atafika tena mahakamani hapo Ijumaa wiki hii, siku ambayo pia Aveva na Kaburu watafikishwa.
  Hans Poppe alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam wakati akitokea nchini Marekani alipokwenda kwa matibabu.
  Zacharia Hans Poppe baada ya kuachiwa kwa dhamana leo Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam

  Anajumuishwa katika kesi ya utakatishaji fedha na kughushi nyaraka inayowakabili Aveva na Kaburu, ambao wamekuwa wakisota rumande tangu Julai 13, mwaka jana baada ya kukamatwa na kushikiliwa na TAKUKURU tangu Juni 29.
  Septemba 15, mwaka huu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alitangaza kuwa yeyote atakayewapata mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe na mwenzake Frank Lauwo atapata zawadi nono.
  Jenerali Mbungo alisema kwamba Hans Poppe yeye alitoa taarifa za uongo kwenye Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwamba Simba SC walinunua nyasi za bandia kutoka kampuni moja ya China kwa thamani ya dola za Kimarekani 40,0577 wakati si kweli. 

  Evans Aveva na Gaoffrey Nyange 'Kaburu' wataendelea kusota rumande kwa sababu mashitaka yao hayana dhamana

  “Lakini uhalisia kamili ni kwamba, zile nyasi zilinunuliwa kwa dola 109,499. Nia hapa ilikuwa ni kutolipwa mapato yanayotakiwa kulipwa TRA, Franklin Peter Lauwo yeye huyu bwana alipata huu ukandarasi kwa njia ya rushwa, kwa sababu alikuwa hana sifa, alikuwa si mkandarasi aliyesajiliwa,”alisema Jenerali Mbungo. 
  Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.
  Wanadaiwa, kuwa  Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE AACHIWA KWA DHAMANA YA SH MILIONI 30 BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA 10 LEO KISUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top