• HABARI MPYA

    Tuesday, October 16, 2018

    POLISI YAMUACHIA KWA DHAMANA MANARA NA WENGINE 18 WALIOKAMATWA KUHOJIWA JUU YA MO DEWJI KUTEKWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    JESHI la Polisi nchini limemuachia kwa dhamana Msemaji wa klabu ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ya Dar es Salaam aliyekuwa anashikiliwa kwa mahojiano juu ya kutekwa kwa mfanyabiashara bilionea, Mohammed ‘Mo’ Dewji. 
    Manara ni kati ya watu 19 walioachiwa kwa dhamana miongoni mwa watu 26 waliokuwa wakihojiwa kuhusiana na tukio la kutekwa Dewji, ambaye yuko mbioni kuwa mwanahisa mkuu wa klabu ya Simba.
    Na hiyo inafuatia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kulitaka Jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wake ili lisiwashikilie washukiwa kwa zaidi ya saa 24. 
    Msemaji wa klabu ya Simba SC, Hajji Manara ameachiwa kwa dhamana  

    Aidha, watu hao wanaachiwa siku moja tu baada ya familia ya Mo Dewji kutangaza zawadi ya Shilingi Bilioni 1 yeyote atakayesaidia kupatikana kwa mpendwa wao huyo aliyetekwa Oktoba 11, mwaka huu.
    Baba mdogo wa Mo Dewji, Azim Dewji ambaye pia ni mfadhili wa zamani wa Simba SC, alitoa ofa hiyo jana katika mkutano na Waandishi wa Habari jengo la Golden Jubilee Towers ghorofa ya 20 mtaa wa Ohio, Posta mjini Dar es Salaam.
    Dewji alisema kwamba Mwenye taarifa anaweza kuwasiliana na mwanafamilia, Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478, 0784783228 na email ya findmo@metl.net.
    Dewji mwenye umri wa miaka 43 alitekwa Alhamisi asubuhi akiwa anaingia katika gym ya Collessium eneo la Masaki mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi baada ya watu wasiojulikana kufyatua risasi hewani mfululizo wakati bilionea huyo anateremka kwenye gari yake kabla ya kumbeba na kumpakia kwenye gari lao na kutokomea naye kwa kasi.
    Mohammed, mtoto wa mfanyabiashara wa siku nyingi, Gulamabbas Dewji – ni rais wa makampuni MeTL Group yaliyoasisiwa na baba yake huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM kati ya mwaka 2005 na 2015. 
    Februari mwaka huu ilielezwa utajiri wa Dewji unafikia dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hivyo kushika nafasi ya 17 katika orodha ya matajiri wa Afrika na kuwa mfanyabiashara kijana tajiri zaidi.
    Kwa sasa, Mo Dewji yuko mbioni kuwa mmiliki wa klabu ya Simba kufuatia mkutano wa wanachama wa Desemba 3, mwaka jana kuazimia kumfanya bilionea huyo kuwa mwanahisa mkuu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
    Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POLISI YAMUACHIA KWA DHAMANA MANARA NA WENGINE 18 WALIOKAMATWA KUHOJIWA JUU YA MO DEWJI KUTEKWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top