• HABARI MPYA

  Thursday, October 18, 2018

  LIGI KUU YA TANZANIA BARA YAREJEA KESHO BAADA YA WIKI MBILI ZA KUPISHA MECHI ZA KIMATAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya soka ya Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kimataifa.
  Kesho kutakuwa na mechi tatu, Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Ndanda FC wataikaribisha Mbeya City ya Mbeya, Uwanja wa Mwadui Complex huko Kishapu mkoani Shinyanga, Mwadui FC wataikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani na Azam FC watakuwa wenyeji wa  African Lyon Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Jumamosi kadhalika kutakuwa na mechi tatu, Tanzania Prisons wakianza na Singida United ya Singida Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Coastal Union na JKT Tanzania ya Dar es Salaam Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza.
  Azam FC watakuwa wenyeji wa  African Lyon kesho Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

  Mechi nyingine tatu zitafuatia Jumapili, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwakaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Lipuli FC wakiwakaribisha Kagera Sugar ya Bukoba Saa 8:00 mchana Uwanja wa Samora mjini Iringa na Mbao FC wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro Saa 10: 00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Hadi sasa Azam FC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 18 za mechi nane, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar pointi 17 mechi tisa, Yanga SC pointi 16 mechi sita, Singida United pointi 16 pia mechi tisa na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 14 za mechi saba.
  Hali ni mbaya kwa Mwadui FC ambao baada ya mechi nane, wana pointi tano, nyuma ya Alliance FC pointi sita mechi tisa, sawa na African Lyon na Tanzania Prisons. Biashara United ya Mara, nayo pia ina pointi sita, lakini za mechi nane.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LIGI KUU YA TANZANIA BARA YAREJEA KESHO BAADA YA WIKI MBILI ZA KUPISHA MECHI ZA KIMATAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top