• HABARI MPYA

  Friday, October 12, 2018

  KILA LA HERI TAIFA STARS, USHINDI WA UGENINI UNAWEZEKANA DHIDI YA CAPE VERDE PRAIA LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania leo inateremka kwenye Uwanja wa Taifa mjini Praia, Cape Verde kumenyana na wenyeji katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 nchini Cameroon.
  Mchezo huo unaotarajiwa kuanza Saa 2:00 usiku wa leo, utaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya ZBC 2, moja ya chaneli nyingi zilizopo kwenye king’amuzi cha Azam TV.  
  Huo utakuwa mchezo wa pili tu kwa kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike tangu ajiunge na Taifa Stars mapema Agosti, baada ya awali kupata sare ya 0-0 ugenini na Uganda mjini Kampala mapema mwezi uliopita.  
  Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.

  Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa mazoezini jana jioni Uwanja wa Taifa mjini Praia 

  Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. Ikumbukwe, Uganda watakuwa wenyeji wa Lesotho Jumamosi mjini Kampala.
  Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
  Kikosi cha Taifa Stars kinatarajiwa kuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Kelvin Yondani, Abdi Banda, Himid Mao, Simon Msuva, Feisal Salum, Mbwana Samatta, John Bocco na Thomas Ulimwemgu.
  Katika benchi wanaweza kuwapo; Beno Kakolanya, Hassan Kessy, Salum Kimenya, Paulo Ngalema, Aggrey Morris, David Mwantika, Mudathir Yahya, Farid Mussa, Yahya Zayed, Rashid Mandawa na Shaaban Iddi Chilunda.
  Kila la heri Taifa Stars. Ushindi ugenini unawezaka leo Praia. Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA STARS, USHINDI WA UGENINI UNAWEZEKANA DHIDI YA CAPE VERDE PRAIA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top