• HABARI MPYA

  Sunday, November 05, 2017

  ‘BAO LA UTATA’ LAIREJESHA SIMBA KILELENI, YAICHAPA MBEYA CITY 1-0

  Na David Nyembe, MBEYA
  SIMBA SC imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ahmed Kikumbo aliyesaidiwa na Omari Juma wote wa Dodoma na Michael Mkongwa kutoka Njombe, Simba ilipata bao hilo kipindi cha kwanza, likifungwa na winga, Shiza Ramadhani Kichuya. 
  Kichuya alifunga bao hilo dakika ya saba baada ya mabeki wa Mbeya City kusita kumdhibiti wakidhani ameotea kufuatia pasi ndefu ya juu ya kiungo Jonas Mkude. 
  Shiza Kichuya (kulia) akiinua mikono juu kushangilia baada ya kufunga leo Uwanja wa Sokoine. Kushoto ni mtoa pasi ya bao hilo, Jonas Mkude
  Kiungo wa Simba, Jonas Mkude akikamiliaba na wachezaji wa Mbeya City

  Mbeya City walifumuka baada ya bao hilo na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba, lakini safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na beki Mganda, Juuko Murshid ilisimama imara kuondosha hatari zote.
  Sifa zaidi zimuendee mlinda mlango, Aishi Salum Manula aliokoa michomo yote iliyoelekezwa langoni mwake.
  Hata kipa kijana mdogo wa Mbeya City, Fikirini Bakari anastahili sifa kwa kuwazuia Simba kupata mabao zaidi, kwani safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na Mganda, Emmanuel Okwi aliyecheza pamoja na John Bocco kipindi cha kwanza kabla ya kuongezewa na Mrundi, Laudit Mavugo kipindi cha pili.
  Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 19 baada ya kucheza mechi tisa na kupanda kileleni ikiizidi kwa wastani wa mabao tu Azam yenye pointi 19 pia. 
  Baada ya mchezo huo, mshambuliaji mkongwe wa Mbeya City, Mrisho Ngassa alilalamikia uchezeshaji wa refa akisema alikuwa anaionea timu yake uwanjani.;
  Kwa upande wake, Kichuya alisema hakuona kama alikuwa ameotea wakati anafunga kwa sababu alimzunguka kwa mbele beki wa Mbeya City na kwa ujumla aliridhishwa na uchezeshaji wa refa.
  Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Fikirini Bakari, Erick Kyaruzi, Hassan Mwasapili, Ally Lundenga, Sankan Mkandawile, Babu Ally, Mrisho Ngassa, Mohammed Samatta, Mohammed Mkopi/Victor Hangaya dk82, Omary Ramadhani/Iddi Nado dk64 na Eliud Ambokile. 
  Simba SC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, James Kotei, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk88, Muzamil Yassin/Laudit Mavugo dk78, John Bocco, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima/Said Ndemla dk55.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ‘BAO LA UTATA’ LAIREJESHA SIMBA KILELENI, YAICHAPA MBEYA CITY 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top