• HABARI MPYA

  Saturday, March 18, 2017

  MBAO YA KWANZA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF, WAING’OA KAGERA SUGAR KAITABA

  Na Princess Asia, MWANZA
  KLABU ya Mbao FC ya Mwanza imekuwa timu ya kwanza kufuzu Nusu Fainali ya Kombe la 
  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) msimu huu, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Mbao iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, ilicheza vizuri leo Uwanja wa Kaitaba kwenye nyasi bandia na kuwapoteza kabisa wenyeji.
  Salmin Hoza alianza kumtungua mchezaji bora wa Ligi Kuu Januari kwa shuti la mbali dakika ya 42  kabla ya Dickson Ambundo kufunga la pili dakika ya 84.
  Mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC na Simba, Ame Ali ‘Zungu’ akaifungia Kagera bao la kufutia machozi dakika ya 92.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mmoja kati ya Simba SC na wenyeji Madini FC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
  Mechi nyingine za Robo Fainali kati ya Azam FC na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na Yanga dhidi ya Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitapangiwa tarehe.
  Bingwa wa michuano hiyo kwa mujibu wa kanuni, atazawadiwa Sh. Milioni 50 na ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakati bingwa wa Ligi Kuu atacheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBAO YA KWANZA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF, WAING’OA KAGERA SUGAR KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top