• HABARI MPYA

  Wednesday, March 15, 2017

  MADINI WAITUNISHIA MSULI SIMBA SC, WASEMA JUMAPILI PATACHIMBIKA

  Na Clement Shari, ARUSHA 
  TIMU ya soka ya Madini FC ya hapa imesema ipo tayari kuvaana na Wekundu wa Msimbazi, Simba SC Jumapili wiki hii katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Madini watakuwa wenyeji wa Simba SC katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la ASFC Uwanja wa Sheikh Amri Abedin mjini hapa wakihitaji ushindi kusonga mbele.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana, kocha mkuu wa Madini FC 
  Abdalah Juma amesema kwamba kikosi chake kipo kamili kuwavaa Simba siku ya jumapili na hakuna majeruhi yeyote katika kikosi chake.
  Madini FC ipo tayari kuvaana na Simba SC Jumapili wiki hii katika Robo Fainali ya Kombe la ASFC

  Amesema kwamba kikosi chake kipo kambini kujiandaa na mchezo huo na amewataka mashabiki wa soka wa mkoani Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ya Madini.
  Akiongea kwa tahadhari kuelekea mchezo huo, kocha Juma amesema anaamini kwa uwezo wa mwenyezi Mungu atashinda pambano hilo, kwani katika mchezo wa soka chochote chaweza kutokea licha ya Simba kuwa timu kubwa na inayoheshimika nchini na barani Afrika.
  Kwa upande wao, mashabiki wa soka mkoani hapa wameonekana kuusubiria mchezo huo kwa hamu kubwa kutokana na mkoa wa Arusha kukosa timu inayoshiriki Ligi  
  Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa takribani miaka mitatu sasa.
  Madini ipo Ligi Daraja Tanzania Bara na kufikia hatua ya robo fainali ya michuano hoyo inayorushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Azam, ilizitupa nje JKT Oljoro ya  
  Arusha, Panone ya Kilimanjaro na JKT Ruvu ya Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MADINI WAITUNISHIA MSULI SIMBA SC, WASEMA JUMAPILI PATACHIMBIKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top