• HABARI MPYA

  Sunday, March 19, 2017

  KINACHOITESA YANGA KINAONEKANA KABISA, WAENDELEE KUPAMBANA TU

  SAFARI ya Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana imefikia tamati baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini.
  Yanga imeshindwa kutimiza ndoto za kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili baada ya mwaka 1998.
  Na sasa itajaribu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo, ikitokea Ligi ya Mabingwa.
  Hiyo ni baada ya jana kutoa sare ya 0-0 na wenyeji, Zanacio jioni Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia.
  Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inatolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Yanga wataumia zaidi kwa kutolewa na Zanaco, kwani bao la kusawazisha la Wazambia hao Dar es Salaam lililopatikana dakika ya 78  kupitia kwa mshambuliaji wake Mghana, Attram Kwame lilikuwa la kuotea.
  Na pamoja na hayo, wachezaji wa Yanga walikuwa wamezubaa kusubiri wapinzani wao watoe nje mpira kiungwana (Fair Play) baada ya mchezaji mwenzao, Obrey Chirwa kuangushwa.
  Siku hiyo, Yanga ilitangulia kwa bao la winga Simon Happygod Msuva dakika ya 39 baada ya kuwachambua mabeki wa Zanaco kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mzambia, Justin Zulu.
  Na ushindi huu unaifanya Zanaco iendeleze rekodi ya kuitupa nje Yanga kwenye michuano ya Afrika, baada ya mwaka 2006 pia kuwatoa katika hatua kama hii ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-2, wakishinda 2-0 Lusaka baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam. 
  Yanga sasa itamenyana na timu iliyofuzu hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho kuwania tikeit ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, wakati Zanaco inakwenda moja kwa moja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
  Pamoja na kutolewa, hali halisi ya michezo yote miwili, Dar es Salaam na Lusaka inaonyesha Yanga bado ni timu bora.
  Bao la kuotea walilofungwa Dar es Salaam ndilo linawaondoa kwenye mashindano na bila shaka yule refa atajisikia vibaya kwa makosa aliyoyafanya.
  Pamoja na hayo, Yanga ipo katika wakati mgumu hivi sasa kifedha, kufuatia Mwenyekiti na mfadhili wake, Yussuf Manji kuingia matatizoni na Serikali.
  Wachezaji wa Yanga morali imeshuka kutokana na hali halisi ya klabu jambo ambalo limewafanya katika Ligi Kuu wasiwe na matokeo mazuri.
  Walishindwa kuifunga Simba pungufu iliyompoteza beki Janvier Bokungu Februari 25 na licha ya kuongoza kwa bao la penalti la Simon Msuva kipindi cha kwanza, wakafungwa mabao mawili dakika za mwishoni na kulala 2-1.
  Washambuliaji wote wanne wa Yanga ni majeruhi na tangu Januari wamekuwa wakicheza kwa kulazimishwa tu na bahati mbaya zaidi mechi ya jana wote hawakuwepo.
  Hao ni Mrundi Amissi Tambwe, Mzimbabwe Donald Ngoma na wazalendo Malimi Busungu na Matheo Anthony.
  Huwezi kustaajabu Yanga kutofunga bao ikiwa inacheza bila mshambuliaji hata mmoja na sasa mawinga, Obrey Chirwa na Msuva ndiyo wanatumika katika nafasi hiyo.
  Matatizo ya Yanga yanayonekana mno na huwezi kustaajabu matokeo wanayopata kwa sasa, ni kwa sababu wanapitia katika kipindi kigumu.
  Pamoja na yote, Yanga wanahitaji kuendelea kushikamana hivyo hivyo na kupambana hadi hapo hali itakapokuwa nzuri tena.
  Kwa sasa waelekeze nguvu zao kwenye kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kila la heri Yanga.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KINACHOITESA YANGA KINAONEKANA KABISA, WAENDELEE KUPAMBANA TU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top