• HABARI MPYA

    Wednesday, February 10, 2016

    WASAUZI WAIKWAMISHA YANGA KUWAHI MAURITIUS, SASA KUONDOKA DAR IJUMAA

    KIKOSI KINACHOKWENDA MAURITUS;
    Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
    Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani.
    Viungo; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger) na Deus Kaseke.
    Washambuliaji; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).
    BENCHI LA UFUNDI; 
    Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi)
    Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi
    Kocha wa Makipa; Juma Pondamali
    Daktari; Nassor Matuzya
    Meneja; Hafidh Saleh
    Mchua Misuli; Jacob Onyango
    Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC sasa itaondoka Dar es Salaam Ijumaa kwenda Mauritius kwa ndege maalum ya kukodi, ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim. 
    Yanga SC ilipanga kuondoka leo, lakini kutokana na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SA) kushindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda Curepipe, Mauritius imeahirisha safari hadi keshokutwa.  
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba ndege ya kuunganisha iliyopatikana leo ingewaweka karibu kutwa nzima Uwanja wa Ndege wa O Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini, hivyo wameona ingewachosha wachezaji.
    Hata hivyo, Muro amesema safari ya Ijumaa itakuwa ya moja kwa moja kwenda Mauritius na timu sasa itaendelea na mazoezi Dar es Salaam kwa siku mbili hizi. 
    "Kamati ya mashindano imeona ni busara timu kuondoka ijumaa kwa ndege maalum ya kukodi itakayobeba kikosi kutoka Dar es Salaam moja kwa moja hadi Mauritius na kisha ndege hiyo itaisubiri timu hadi siku ya Jumamosi itakapomaliza mechi na kuondoka Jumamosi hiyo hiyo usiku kuelekea kambini kisiwani Pemba ambako itaweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba Februari 20,"amesema Muro. 
    Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi kuanzia Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe na Pluijm amebebea karibu kikosi chake chote, akiacha wachezaji watatu tu.
    Hao ni kipa wa tatu, Benedicto Tinocco, kiungo Godfrey Mwashiuya na mshambuliaji Matheo Anthony. 
    Wachezaji waliokuwa majeruhi, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Amissi Tambwe wote watasafiri na timu.
    Mkuu wa Msafara ni Ayoub Nyenzi, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati upande wa viongozi wanakwenda Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit na Muro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WASAUZI WAIKWAMISHA YANGA KUWAHI MAURITIUS, SASA KUONDOKA DAR IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top