• HABARI MPYA

    Friday, February 12, 2016

    TFF YAITOA NGORONGORO MATAIFA YA AFRIKA ILI KUJENGA UPYA MSINGI WA SOKA YA VIJANA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeitoa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ili kujenga msingi imara wa soka ya vijana, badala ya kuchukua wachezaji ambao haina rekodi zao halisi.
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba wanataka kujenga msingi mpya wa soka ya vijana nchini.
    “Kwa sasa ukisema uunde U-20 ina maana utachukua wachezaji wa klabu mbalimbali kulingana na rekodi zao za umri. Na tumekuwa tukifanya hivyo kwa muda mrefu, lakini hatufiki popote,”amesema Malinzi.
    “Sasa hivi tunajenga msingi mpya imara wa soka ya vijana kuanzia timu ya vijana chini hya umri wa miaka 13 ambayo tayari ipo kambini Mwanza. Na hii ya U-15 tuliyoanza nayo mwaka jana, ambayo sasa itacheza michuano ya U17,”.
    “Kuanzia hapa sasa, ndiyo tutakuwa na timu za vijana za U-17, U-20 na U-23 kwa ajili ya kucheza mashindano yote, kwa sababu tayari tutakuwa na msingi unaoeleweka,”amesema Malinzi.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema wanajenga msingi imara wa soka ya vijana

    Pamoja na hayo, Malinzi amesema kwamba wakati mkakati huo ukiendelea na TFF inaendelea kutafuta wadhamini na wafadhili kwa ajili ya timu za vijana na wanawake.
    “Mechi moja ya kufuzu fainali za vijana au za wanawake gharama zake ni zaidi ya dola (za Kimarekani) 70,000 (zaidi ya Sh. Milioni 140), lakini uwanjani watu hawaendi na hupati fedha, wakati huna wafadhili wala wadhamini,”.
    “Kwa nchi za wenzetu zilizoendelea ambazo ama vyama vyake vya soka vina uwezo kifedha, au vinasaidiwa na Serikali zao, vinaweza kushiriki mashindano yote, ila kwa sisi kwa kweli ni vigumu,”amesema Malinzi.
    Rais huyo wa TFF amesema kwamba wanajitahidi kuhakikisha kunakuwa na mifuko maalum ya fedha kwa ajili ya soka ya vijana, ili ifike wakati timu zote zianze kushiriki vyema.  
    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wiki hii limetoa ratiba ya mechi za kufuzu za michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na miaka 20.
    Katika mbio za fainali za U-17 nchini Madagascar mwaka 2017, Tanzania imepangwa kuanza na Shelisheli Juni mwaka huu, wakati kwenye U-20 ambayo fainali zake zitafanyika Zambia Ngorongoro Heroes haimo.   
    “Sikuisajili Ngorongoro, nimeingiza Serengeti tu, na ukiangalia si Tanzania tu, nchi nyingi sasa hivi haziingizi timu zote za vijana kwenye mashindano, zinachagua pale ambapo zinaona ziko tayari tu,”.
    “Ni nchi chache sana kama Afrika Kusini labda au Ivory Coast, Cameroon na Nigeria ambazo zina uwezo kwa maana zote, zina timu na msingi imara wa soka ya vijana pamoja na fedha pia,”amesema Malinzi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAITOA NGORONGORO MATAIFA YA AFRIKA ILI KUJENGA UPYA MSINGI WA SOKA YA VIJANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top