• HABARI MPYA

    Thursday, February 11, 2016

    MOROCCO 'YAMTIMUA KISTAARABU' ZAKI BAADA YA MATOKEO MABAYA

    KOCHA Badou Zaki (pichani kulia) amebwaga manyanga timu ya taifa ya Morocco kwa sababu za kawaida, imesema taarifa ya Shirikisho la Soka Morocco (FRMF) leo."Baada ya miezi 20 ya matokeo yasiyoridhisha na kusuasua, shirikisho limekubaliana na Zaki kuvunja Mkataba kwa sababu za kawaida,"imesema taarifa ya shirikisho na kuongeza kwamba kocha mpya atatajwa siku chache zijazo.
    Kipa huyo wa zamani wa kimataifa, Zaki mwenye umri wa miaka 56, alipewa ukocha wa Morocco kwa mara ya pili Mei mwaka 2014, lakini timu haikufanya vizuri na ikatolewa hatua ya makundi katika Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) hivi karibuni.
    Awali, Zaki aliiongoza Morocco kwa miaka mitatu kuanzia 2002, ikifungwa na Tunisia katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004.
    Tetesi zinasema, kocha wa zamani wa Zambia na Ivory Coast, Herve Renard mwenye umri wa miaka 47, ambaye amefukuzwa na klabu ya Lille ya Ufaransa mapema msimu huu anatarajiwa kupewa mikopba ya kufundisha Morocco.
    Gazeti la michezo la kila siku la Ufaransa, L'Equipe limesema kwamba habari za ndani kutoka FRMF tangu mwezi uliopita zinasema, Renard aliyezipa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Zambia mwaka 2012 na Ivory Coast mwaka jana anapewa nafasi kubwa ya kuwa kocha mpya wa Morocco.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MOROCCO 'YAMTIMUA KISTAARABU' ZAKI BAADA YA MATOKEO MABAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top