• HABARI MPYA

    Wednesday, February 10, 2016

    ZAMALEK YAMTUPIA VIRAGO MIDO BAADA YA KIPIGO CHA AL AHLY JANA MISRI

    VIGOGO wa Misri, Zamalek wamemfukuza kocha wao, Ahmed Hossam, maarufu kama Mido, baada ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa Cairo, Al Ahly.
    Zamalek pia imemfukuza Mkurugenzi wa Soka, Hazem Emam na kumteua Mohamed Salah kuwa kocha wa muda.
    Mido, ambaye pia amechezea Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya England, alikuwa mshambuliaji wa Zamalek kabla ya kustaafu mwaka 2013 na kuteuliwa kuinoa klabu yake hiyo Januari mwaka 2014.
    Lakini baada ya mchezo wa jana uliochezeshwa na refa wa Hungary mwenye umri wa miaka 40, Viktor Kassai aliyechezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2011, ndoa ya Mido na Zamalek imevunjika.

    Kocha Ahmed Hossam 'Mido' amefukuzwa Zamalek baada ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu, Al Ahly jana

    Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab, umbali wa kilomita 200 kutoka mji wa Cairo, jirani na Jiji la Alexandria kwa sababu za kiusalama haikuhudhuriwa na mashabiki ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu huo tangu janga la Port Said Februari mwaka 2012.
    Ahly, inayofundishwa na kocha mzalendo, Abdul Aziz Abdul Shafy ‘Zizo’, sasa inaongoza Ligi ya Misri kwa pointi zake 38, saba zaidi ya wapinzani wao hao baada ya kila timu kucheza mechi 16. 
    Huo ulikuwa mchezo wa 112 kuikutanisha miamba hiyo katika Ligi ya Misri tangu ianzishwe mwaka 1948, Ahly ikishinda mara 40, Zamalek 25 wakati mara 46 zimetoka sare.
    Na hiyo ndiyo miamba inayotawala Ligi ya Misri kwa pamoja ikiwa imetwaa mataji 49 ya ubingwa kati ya 58, huku Ahly ikiongoza kutwaa mara nyingi, 37 wakati Zamalek wamechukua mara 12 tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZAMALEK YAMTUPIA VIRAGO MIDO BAADA YA KIPIGO CHA AL AHLY JANA MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top