• HABARI MPYA

    Wednesday, February 10, 2016

    BODI YA LIGI INACHEMSHA NA KAMATI YA AKINA KABURU, SANGA NAYO...

    HAPANA shaka Ligi Kuu ya England ndiyo inayoongoza kupendwa na kufuatiliwa na wengi miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.
    Ni ligi bora kwa maana zote, ushindani wa timu, ubora wa soka pia na umaarufu.
    Ligi hiyo inaendeshwa na Bodi Maalum, ambayo imeundwa kama Kampuni binafasi, inayomilikiwa na klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu katika msimu husika. 
    Kila moja kati ya klabu 20 zinakuwa na hisa katika Ligi Kuu na hukutana kila mwisho mwa msimu kupanga mikakati na taratibu mbalimbali za msimu mwingine wa Ligi Kuu katika Mkutano maarufu kama AGM.

    Inapofika mwishoni mwa msimu, timu zinazoshuka Daraja hukabidhi hisa zao kwa timu zinazopanda kutoka Daraja la Kwanza, maarufu kama Championship.
    Klabu zinakuwa na fursa ya kupendekeza sheria mpya na mambo mbalimbali katika Mkutano wa mwaka, huku kila klabu ikiwa na kura moja katika michakato ya masuala yote yanayohitaji kupigiwa kura kwa maamuzi. 
    Chama cha Soka England (FA) ndiye msimamizi mkuu wa soka nchini humo ikiwemo Ligi Kuu na Kanuni zake. 
    FA ya England nayo ni mwanahisa maalum katika Ligi Kuu, ambaye hata hivyo haina mamlaka katika uendeshwaji wa kila siku wa Ligi Kuu. 
    Kila mwaka, Ligi Kuu wanawasilisha sheria zao kwa FA ili zihakikiwe na kuidhiniahwa kutumika, na FA ya England inabaki na wajibu wa kusimamia marefa, klabu na wachezaji ndani na nje ya Uwanja katika masuala yote ya kinidhamu, ndani na nje ya Uwanja.
    Huo ndiyo mfumo wa ligi nyingi duniani hivi sasa hata Afrika, vyama vya soka vimejitoa katika kusimamia na kuendesha ligi, vikibaki tu kuendesha na kusimamia moja kwa moja mashindano yake maalum, tu kama FA.
    Nchini Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu sasa nasi Ligi yetu imeundiwa chombo binafasi, mali ya klabu, kiitwacho Bodi ya Ligi Kuu.
    Hakuna tofauti ya kimfumo kwa Bodi ya Ligi ya England na Bodi ya Ligi ya Tanzania Bara, zote zinamilikiwa na klabu.
    Kumekuwa na malalamiko ya bodi kutopewa mamlaka ya moja kwa moja katika masuala yanayohusu ligi, hususan mikataba ya udhamini na kadhalika.
    Lakini pamoja na kuwapo kwa bodi ya ligi, pia kuna chombo kimeundwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kiitwacho Kamati ya Mashindano, nacho pia kinajikuta kinahusishwa na uendeshwaji wa Ligi.
    Kamati ya Mashindano inaundwa na viongozi wa kuteuliwa kutoka klabu mbalimbali mfano Mwenyekiti wake, Injinia Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Simba SC, Makamu wake, Clement Sanga pia ni Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga pia.
    Wajumbe wa Kamati hiyo ni James Mhagama, Stewart Masima, Steven Njowoka na Sheikh Said Mohammed wa Azam FC. 
    Pamoja na kwamba Wajumbe wa Kamati ya Mashindano wamekuwa wakiisukumia lawama Bodi ya Ligi kwa mapungufu yote yanayojitokeza kuhusu mwenendo wa Ligi Kuu, lakini na wao pia wamekuwa wakinyooshewa vidole.
    Inaonekana viongozi wa Simba, Yanga na Azam FC wana nguvu ya moja kwa moja ya kubadilisha mwelekeo wa Ligi Kuu kwa maslahi yao binafsi bila kujali athari zake, tu kwa sababu wana mikono kwenye vyombo hivyo viwili, yaani Bodi ya Ligi na Kamati ya Mashindano.
    Hii imesababisha Ratiba ya Ligi kupanguliwa mara kwa mara, kanuni kutozingatiwa na kadhalika.
    Kwa mfano mwanzoni mwa msimu kulijitokeza mkanganyiko wa kikanuni, klabu ya Simba ikimtumia mchezaji Ibrahim Hajib akiwa ana kadi tatu za njano, kwa madai kuna mabadiliko ya kanuni.
    Simba SC walisema kuna kanuni mpya inaipa fursa klabu kuchagua mechi za mchezaji kukosa akiwa anatumikia adhabu ya kadi.
    Hili lilivuja kutoka kwenye Kamati ya Mashindano na ikadaiwa chanzo kilikuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kaburu ambaye pia ni Makamu Rais wa Simba SC.
    Lakini kumbe suala hilo lilijadiliwa tu na halikupitishwa, lakini Simba SC ikavunja kanuni kutokana na kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ni wao – Kaburu wakaamini mambo yatakuwa kama yanavyotarajiwa.
    Mwisho wa siku, kanuni hiyo haikupitishwa na makosa makubwa yakaingia kwenye kumbukumbu, Simba SC ikivuna pointi tatu haramu kutokana na kumtumia mchezaji mwenye kadi tatu za njano.
    Sahau kuhusu mapungufu yaliyomo ndani ya Bodi ya Ligi Kuu, mfumo wake wa utendaji kuwa mbovu na hata uwajibikaji usioridhisha wa Maofisa walioajiriwa.
    Ipo haja ya kuiboresha Bodi ya Ligi, iwe na sura kama bodi nyingine kongwe katika uendeshaji wa Ligi duniani, mfano Ligi Kuu ya England na pia kuipa Mamlaka kamili, ili TFF wabaki kusimamia sheria na kanuni tu ndani na nje ya Uwanja.
    Tazama ilivyo sasa, unapofikiria suluhisho la mapungufu ya Bodi na Watendaji wake, linakuja suala la Kamati ya Mashindano pia kuchangia kuivuruga ligi yenyewe. Siyo sahihi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BODI YA LIGI INACHEMSHA NA KAMATI YA AKINA KABURU, SANGA NAYO... Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

    PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

    Scroll to Top