• HABARI MPYA

    Sunday, July 13, 2014

    EVANS ELIEZA AVEVA, HILI SI LA KUPUUZIA HATA KIDOGO NDANI YA SIMBA SC

    ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage wiki hii amekabidhi rasmi madaraka kwa kiongozi mpya wa klabu hiyo, Evans Elieza Aveva.
    Rage alikutana na Aveva na baadhi ya Wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji, makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi na kuwakabidhi nyaraka mbaimbali za klabu.
    Pamoja na kukabidhi nayaraka zikiwemo za mikataba tofauti, Rage pia alimpa wosia Aveva.
    Alimuambia, wakati wa kampeni za kuomba Urais wa Simba alipita kwenye matawi na kuwaahidi wanachama kwamba pamoja na mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja, atarejesha umoja ndani ya klabu.

    Rage akamuambia Aveva ahakikishe anatimiza ahadi zake baada ya kuingia madarakani, akianza na kuwasamehehe wanachama zaidi ya 60 walioipeleka klabu hiyo mahakamani wakati wa mchakato wa uchaguzi.
    Ikumbukwe uchaguzi wa Simba SC ulikumbwa na mizengwe mingi- kiasi cha baadhi ya wanachama kwenda kutaka kuuzuia mahakamani ambako, hawakufanikiwa.
    Baada ya kuingia madarakani, Aveva katika Mkutano wake wa kwanza na Waandishi wa Habari akasema kwamba amewasimamisha uanachama, wanachama ambao walikwenda mahakamani.
    Aidha, Aveva akasema mwezi ujao utafanyika Mkutano Mkuu na huko ataliwasilisha suala la wanachama hao lijadiliwe pamoja na la mwanachama mwingine, Michael Wambura ambaye anakabiliwa na kesi kama hiyo.
    Rage amemuunga mkono Aveva kwa hatua aliyoichukua kwanza, akisema kwamba imeinusuru klabu hiyo kufungiwa na FIFA, ambayo haitaki masuala ya soka yapelekwe kwenye mahakama za dola.
    Alisema kama Aveva asingewachukulia hatua wanachama hao, Simba SC ingeonekana ina matatizo na ingekuwa hatarini kufungiwa na FIFA.
    Lakini pamoja na ukweli huo, Rage akamuambia Aveva ahakikishe anarejesha umoja na amani klabuni kama alivyoahidi kwenye kampeni zake.
    Aveva alipigiwa kura za ndiyo na wanachama karibu 1,500, mpinzani wake wa karibu aliambulia kura 300 na ushei, wakati waliokwenda mahakamani hawafiki 70.
    Unaweza kuona Aveva ni mtu anayekubalika kiasi gani Simba SC na anaweza kuwavutia hata hao wengine, iwapo hatakuwa na fikra za visasi dhidi ya anaoamini ni wabaya wake, badala yake akaamua kurejesha umoja klabuni.
    Mengi yamepita wakati wa kampeni, kuna mabango walibebeshwa wanachama, kwa kweli yalikuwa yanaudhi, yanakera, yanadhalilisha na yanashawishi kulipa kisasi.
    Kuna jambo ambalo Aveva anatakiwa kujua leo, kwa muda mrefu nchini kwetu uzoefu umekuwa moja ya sifa za kupewa wadhifa au madaraka ya uongozi.
    Sababu ni kwamba, mzoefu ni ambaye amekwishakutana na mengi, nafsi yake imekomaa, anajua kustahmili, kupuuza na kusamehe- ili asitoke ndani ya mistari.
    Aveva atakumbukwa, na atakuwa kiongozi wa kihistoria ndani ya Simba SC, iwapo katika Mkutano wa mwezi ujao atatumia nafasi yake kama Rais wa klabu, na namna ambavyo anavyoungwa mkono na wanachama wengi kushawishi urejeshwaji wa umoja.
    Umoja ndiyo msingi mkuu wa amani na mafanikio katika jambo lolote, hata mababu zote walinena; “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”. 
    Kaulimbiu ya Simba SC ni; “Nguvu Moja”, na kweli wanachama wote wa klabu hiyo wanapaswa kuunganisha nguvu zao na kuweka tofauti zao pembeni kabisa.
    Migogoro inatokea hadi kwenye taasisi za dini, ndani ya familia, lakini mwisho wa siku suluhu hutafutwa na watu wakazika tofauti zao.
    Hiki ndicho ambacho na Aveva anatakiwa akisimamie ndani ya Simba iwe Nguvu Moja ilete maana yake Msimbazi. Ramadhani Karim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: EVANS ELIEZA AVEVA, HILI SI LA KUPUUZIA HATA KIDOGO NDANI YA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top