• HABARI MPYA

    Monday, July 21, 2014

    HAYA NDIYO MAMBO YA MINZIRO, NI BURUDANI YA ZIADA ZAIDI YA DAKIKA 90 ZA MCHEZO UWANJANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAKOCHA wana vitimbi vyao wanapokuwa wanaongoza timu zao- na mara nyingi ambao husisimua ni wale, ambao huwa hawatulii kwenye viti vyao wakati wa mechi, wakiwapigia kelele wachezaji wao.
    Hawa huwa hawachelewi hata kutukana waamuzi au wakati mwingine hata kuwavaa na kuwashambulia- kwa sababu wana kile kitu kinaitwa munkari.
    Walimu wengine baada ya kumalizana na wachezaji wao vyumbani, wanapoingia uwanjani huwaacha hadi baada ya kumalizika kwa ngwe ya kwanza azungumze nao tena.
    Hapa anasema nao; Cheza mpira, namna hiyoo
    Hapa anamshangaa refa; Wewe refaa wewee
    Yowe la nguvu, kutoka Chamazi Kariakoo walimsikia
    Hapa anashangaa, au; Ameweka pozi anaangalia mchezo

    Lakini Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro ‘Majeshi’ hayuko hivyo. Anatoka kuzungumza na wachezaji chumbani, lakini mchezo ukianza kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho anawapia kelele.
    Tena si kelele tu, atanyoosha mikono, ataibadilisha sura yake, ataruka ruka, atakwenda na kurudi kama mtu aliyesusa- lakini atainuka tena na hali itaendelea kuwa hivyo hadi mwisho wa mchezo.
    Kwa wachezaji wagumu kuelewa, mwalimu anayewafaa ni Minziro kwa sababu anawakumbusha majukumu na wajibu wao muda wote wa mchezo.
    Kama amesusa, lakini bado yupo kazini
    Mishipa ya shingo inasaidia kazi koo kupiga kelele 

    Lakini kwa mashabiki, Minziro huwa burudani ya ziada zaidi ya ule mchezo unaoendelea uwanjani kwa vitimbi vyake. Sauti yake nyembamba na kali pekee ni burudani tosha anapowapigia kelele wachezaji wake. “Cheza mpira, nini hiyooo, haifaai” Aaaa weweee refaa weweee,”. Ni raha tu.
    Baada ya kuwa kocha Msaidizi wa klabu yake ya zamani, Yanga SC kwa takriban miaka minne, Minziro amerudi kuwa kocha Mkuu wa Ligi Kuu kupitia klabu ya JKT Ruvu.
    Wiki iliyopita Minziro aliiongoza timu hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC Uwanja wa azam Complex, Chamazi, Dar es salaam ambao alipoteza kwa mabao 2-1.
    Siku hiyo, beki huyo wa zamani wa Yanga na timu ya mkoa wa Dar es Salaam ‘Mzizima’ alipiga kelele mno na kufanya kila aina ya vitimbi alivyoweza katika kufikisha ujumbe kwa wachezaji wake.
    Ilisaidia, mwanzoni ilionekana kama JKT ingepigwa nyingi, baada ya kukubali mabao mawili ya haraka haraka, lakini baadaye timu hiyo ya Jeshi ka Kujenga Taifa ikasimama imara na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi katika mchezo ambao wangeweza kupata sare au hata kushinda. Hayo ndiyo mambo Minziro, anapokuwa kazini hataki mzaha.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAYA NDIYO MAMBO YA MINZIRO, NI BURUDANI YA ZIADA ZAIDI YA DAKIKA 90 ZA MCHEZO UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top