• HABARI MPYA

    Thursday, July 24, 2014

    WAZEE WA REAL MADRID WATINGA KWA ‘RAIS WA DAR’, AAHIDI KUWAPA TAFU LA NGUVU

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Maandalizi ya ziara ya kikosi cha magwiji wa Real Madrid ya Hispania, leo imemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick na kumuelezea rasmi juu ya tukio hilo la mwezi ujao.
    Ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Farough Baghozah, Kamati hiyo ilifika ofisi ya Mkuu ya Mkoa wa Mkoa, Ilala, Dar es Salaam, Meckysadick ambaye alifurahishwa kwa ujumla na jambo hilo.
    Meneja ziara wa magwiji hao wa Real, Dennis Ssebo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba walipokewa vizuri na Mkuu wa Mkoa ambaye ameahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika tukio zima hilo.
    Kutoka kulia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Farough Baghozah na Wajumbe, Evarist Hagila na Saad Kawemba

    “Tulipokewa vizuri, na Mkuu wa Mkoa kwa heshima na taadhima ameahidi kutupa ushirikiano wa kutosha kabisa,”amesema Ssebo. 
    Wachezaji waliotamba kuanzia La Liga, wakacheza ligi nyingine za Ulaya, Kombe la Ulaya, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia waliowahi kuchezea Madrid watakuja nchini Agosti 22.
    Katika ziara hiyo, pamoja na kucheza mchezo wa kirafiki na kikosi maalum cha wachezaji nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kupanda mlima Kilimanjaro.
    Real Madrid inakuja nchini kwa mwaliko wa kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Farough Baghozah.
    Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja na Real nchini ni pamoja na Wanasoka Bora wa zamani wa Dunia, Mfaransa Zinadine Zidane, Mreno Luis Figo na Mbrazil, Ronaldo Lima.
    Magwiji hao wa Real tayari wamekwishafanya matangazo ya ziara yao nchini wakisema wana hamu mno ya kukanyaga ardhi ya Tanzania.
    Kampuni ya Vodacom Tanzania ni miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza kudhamini ziara pamoja na Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza Bahari Beach.
    Wito umetolewa kwa makampuni zaidi kujitokeza kudhamini ziara hiyo ya kihostoria nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZEE WA REAL MADRID WATINGA KWA ‘RAIS WA DAR’, AAHIDI KUWAPA TAFU LA NGUVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top