• HABARI MPYA

    Wednesday, July 23, 2014

    FRIENDS OF SIMBA WAKIRUDI NA MAWAZO YA ‘MWAKA 47’, ITAKULA KWAO

    SIMBA SC ilitawala soka ya Tanzania mwanzoni mwa muongo uliopita hadi katikati.
    Wakati huo, kundi maarufu la wanachama wa klabu hiyo, Friends Of Simba lilikuwa likiisimamia timu na kuisaidia kwa hali na mali.
    Kundi hilo lilikuwa linafanya hivyo kwa kushirikiana na uongozi uliokuwa madarakani na hakuna siri- mafanikio ya klabu hiyo wakati huo yalitokana na wao.
    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC iliwafunga watani wao, Yanga SC mfululizo mchana na siku na kwenye mashindano yote.
    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC ilitwaa mataji mengi mfululizo, kuanzia Ligi Kuu, Ligi ya Muungano, Kombe la FAT, Nyerere na hata Kombe la Kagame.

    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kuitoa kwenye mashindano timu ya Misri, baada ya mwaka 2003 kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek na kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 
    Lakini Friends walishindwa kuendelea na kazi yao nzuri waliyokuwa wakiifanya, baada ya kuingia uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage ambaye hawakuwahi kuiva naye chungu kimoja.
    Mambo yakawa magumu Simba SC wakati wa utawala wa Rage, hadi F.O.S. walipoamua kujipanga kuingia wao wenyewe madarakani.
    Awali walitaka kumsimamisha Zacharia Hans Poppe kugombea Urais, lakini ikatokea mizengwe wakaamua kumsimamisha Evans Eliaza Aveva ambaye alishinda.
    Aveva sasa Rais wa Simba SC na maana yake klabu imerudi mikononi mwa timu ya mafanikio, Friends Of Simba.
    Pamoja na ukweli huo, F.O.S. wanapaswa kufanya tathmini ya wakati ambao waliiwezesha klabu hiyo kutawala soka ya Tanzania na kufananisha na wakati huu, ambao Yanga na Azam wanatamba.
    Wanachama na wapenzi wa Simba SC wana matumaini makubwa sana baada ya ushindi wa Aveva ambao ndio ushindi wa F.O.S.
    Kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic amesema jana baada ya kusaini Mkataba mpya kwamba Simba SC itakuwa timu bora msimu ujao.
    Na Makamu wa rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amemuambia ubingwa wa Ligi Kuu ndiyo msalaba wake katika msimu huo.
    Lakini haya si mambo mepesi mbele ya kocha huyo wala F.O.S., kwa sababu ya hali halisi katika soka ya Tanzania kwa sasa ukilinganisha na muongo uliopita.
    Wakati Friends wanaifanya Simba itawale soka ya Tanzania, Yanga SC ilikuwa timu hohe hahe haina uwezo wa kusajili wachezaji wazuri wala kocha wa maana, ama kuwalipa vizuri wachezaji au hata kufanya fitina nyingine za soka pamoja na maandalizi mazuri.
    Wachezaji wote wazuri walikuwa wanakwenda Simba SC na Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao waliachwa na timu zao, au kuita chipukizi kuwafanyia majaribio.
    Zaidi ya Yanga, timu nyingine iliyokuwa vizuri wakati huo ilikuwa Mtibwa Sugar, lakini nayo haikuonekana kuwa na dhamira ya kushindana kama ilivyokuwa siku za mwanzoni za ujio wake Ligi Kuu ilipoweza kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo 1999 na 2000.     
    Unaweza kuona Friends Of Simba walipita katika njia nyepesi mno kuifikisha Simba SC katika kilele cha mafanikio.
    Vipi wakati huu? Azam ni bingwa, aliyemvua taji Yanga na hizo ndizo timu bora kwa sasa nchini. 
    Azam ni timu ya bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake wakati Yanga SC inajivunia Mwenyekiti wake, milionea Yussuf Manji.
    Yanga SC ya sasa si hohe hahe tena, inasajili wachezaji wa maana tena inaipiku Simba SC sokoni- inaajiri makocha wa maana, wachezaji wanalipwa na kuhudumiwa vizuri.
    Maandalizi ya timu yanakuwa mazuri kiasi cha kwenda hadi kuweka kambi Ulaya.
    Kuna Mbeya City ambayo imepanda Ligi Kuu msimu uliopita na kuonyesha ushindani wa hali ya juu katika Ligi Kuu kiasi cha kuiangushia Simba SC nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.
    Timu zote zilizoshika nafasi tatu za juu msimu uliopita, Azam FC, Yanga SC na Mbeya City zimejidhatiti kuelekea msimu ujao kwa usajili na maandalizi.
    Simba SC inaota kuzipiku timu zote hizo na kunyakua ubingwa- hilo si jambo jepesi na wanatakiwa kujipanga haswa. Friends Of Simba lazima waje kivingine, na mikakati na mbinu mpya ili wafanikiwe kuirudisha kwenye mstari Simba SC, lakini wakija na mawazo ya wakati ule walipoiwezesha timu kutawala kiulaini soka ya Tanzania, itakula kwao. Ramadhani karim. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FRIENDS OF SIMBA WAKIRUDI NA MAWAZO YA ‘MWAKA 47’, ITAKULA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top