• HABARI MPYA

    Saturday, July 26, 2014

    POLISI WAENDEA MBIO SAINI YA DANI MRWANDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Polisi Morogoro, Mohammed ‘Rishard’ Adolph amesema kwamba yuko katika mpango wa kumsajili mshambuliaji mkongwe, Dani Mrwanda kuongeza nguvu katika kikosi chake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ligi Kuu ya Bara inatarajiwa kuanza Septemba 20 mwaka huu na Polisi inakimbizana na muda kukamilisha usajili wake, kabla ya dirisha kufungwa rasmi Agosti 17, mwaka huu.
    “Tupo kwenye mazungumzo na mipango kwa ujumla ya kumsajili Dani, kama mambo yatakwenda vizuri, basi tutakuwa naye,”amesema kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, aliyewika klabu za Pan Africans na Yanga SC.  
    Dani Mrwanda kulia akiwa na beki wa Polisi Moro, Lulanga Mapunda jana

    Lakini BIN ZUBEIRY inafahamu kwamba Mrwanda ametaka kusajiliwa ili kucheza mzunguko wa kwanza tu wa Ligi Kuu, kwa kuwa atarejea Vietnam Januari mwakani kuendelea kucheza soka ya kulipwa.
    Mrwanda hataki kukaa bure kipindi hiki amacho yupo nyumbani kwa mapumziko na anataka ahamishiwe timu ya Morogoro kucheza kwa mkopo hadi Januari. Tayari amekwishaanza kujifua na timu hiyo na jana aliifungia bao moja katika sare ya 1-1 na Azam FC. 
    Polisi imeweka kambi katika Chuo cha Polisi, Kurasini Dar es Salaam ikijifua na kucheza michezo ya kirafiki kujiandaa na Ligi Kuu baada ya kupanda tena msimu huu.
    Adolph aliyekuwemo kwenye kikosi cha Tanzania, Taifa Stars kilichocheza Fainali pekee za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria anaonekana kupanua kuifanya Polisi iwe tishio Ligi Kuu msimu ujao. 
    Kocha Mohammed 'Adolph' Rishard amepania kuifanya Polisi iwe tishio katika Ligi Kuu msimu ujao 

    Wiki hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili kwa wiki mbili ili kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa na sasa hatua ya kwanza ya usajili inakamilika Agosti 17 mwaka huu badala ya Agosti 3 ya awali.
    Kutokana na marekebisho hayo, kipindi cha uhamisho kinakamilika Agosti 17 mwaka huu wakati pingamizi itakuwa kati ya Agosti 19 hadi 26 mwaka huu.
    Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2 mwaka huu.
    Uhamisho wa kimataifa, usajili wa wachezaji huru, na utatuzi wa dosari za usajili unatakiwa uwe umekamilika kufikia Septemba 7 mwaka huu. Uthibitisho wa hatua ya mwisho ya usajili utafanywa Septemba 15 mwaka huu.
    Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015 itaanza Septemba 20 mwaka huu, na ratiba itatolewa mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POLISI WAENDEA MBIO SAINI YA DANI MRWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top