• HABARI MPYA

    Sunday, July 27, 2014

    KWA KIASI FULANI, TUMEFANIKIWA KATIKA DHANA YA UWEKEZAJI KWENYE SOKA YA VIJANA, LAKINI...

    ITISHA mashindano ya vijana Tanzania wakati wowote kwa sasa, iwe chini ya umri wa miaka 15, miaka 17 hata 20, zitajitokeza timu za kutosha na zilizo tayari kushiriki.
    Mpira unachezwa kwa kiasi kikubwa kwa sasa Tanzania, kuanzia mijini na vijijini na haya ni matunda ya mashindano ya vijana yaliyo katika mfumo wa kitaifa kama Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars.
    Inakuwa rahisi mno kwa klabu za Ligi Kuu kupata wachezaji wa kuunda timu zao za vijana. Inakuwa rahisi mno katika uundwaji wa timu za taifa za vijana- kwa sababu tayari vipaji vimekwishaibuliwa.

    Leo huhitaji kufoji mchezaji kijeba katika mashindano ya vijana- kwa sababu wachezaji wenyewe vijana halisi wapo.
    Tumetoka mbali, wakati ambao taifa zima lilitegemea shule ya Makongo pekee kama kituo cha kulea vipaji vya vijana.
    Leo hii shule kadhaa nchini zinasaidia mpango wa soka ya vijana, kuna vituo vingi vijana wanacheza. Kuna timu nyingi za vijana nchini, tena za ushindani.
    Baadhi ya klabu zina programu nzuri za soka ya vijana mfano Azam FC na timu za majeshi, hususan za Jeshi la Kujenga la Taifa (JKT).
    Lakini bado tunakabiliwa na tatizo moja kubwa la msingi- tunaibua vipaji kwa wingi, baada ya hapo inakosekana fursa ya kuwaendeleza vijana.
    Hakuna mashindano maalum ya vijana kucheza kwa muda mrefu, ili kuwajengea uwezo wa kushindana na kuwakomaza kwa ujumla.
    Kanuni za Ligi Kuu zinaelekeza kila klabu inapaswa kuwa na timu ya vijana, tena wachezaji wanasajiliwa rasmi kwa ajili ya kucheza ligi yao.
    Lakini ligi hiyo ya vijana imeshindwa kufanikiwa kwa sababu, timu hazisafiiri kama ilivyo kwa timu za wakubwa, zinacheza mechi nyumbani tu.
    Kwa sababu Dar es Salaam kuna Simba, Yanga, Azam, JKT Ruvu, basi na timu za vijana na klabu hizo zitakutana kabla ya wakubwa zao kucheza mechi za Ligi Kuu.
    Kikubwa kinachoelezwa na klabu ni kwamba, hawana uwezo wa kusafirisha timu za vijana kwa sababu ligi hiyo ya vijana haina mdhamini.
    Matokeo yake sasa, klabu za Ligi Kuu timu zao zote za vijana hukutanishwa katika mashindano ya wiki mbili ya mtoano kutafuta bingwa, maarufu kama Kombe la Uhai.
    Baadhi ya timu zitaweza kushiriki mashindano mengine kama Kombe la Rollingston ambayo pia ni michuano ya mtoano ya wiki mbili.
    Mchezaji akijirudia kwenye Kombe la Uhai mara tatu, tayari ataitwa mzee, kwa sababu amecheza mashindano hayo kwa miaka mitatu. Lakini hatujiulizi katika kipindi hicho amecheza mechi ngapi?
    Tumekuwa tukiona timu zetu za vijana za taifa, hazifanyi vizuri katika michuano ya kufuzu kwa Fainali za Afrika tu kwa sababu wachezaji wake wanazidiwa uwezo na wenzao.
    Wanazidiwa uwezo na wenzao ambao wanaonekana wamekomaa zaidi kisoka, japokuwa kiumri hakuna tofauti- sababu wenzao wanacheza sana mashindano, kitu ambacho wao wanakosa.
    Wiki iliyopita tuliona U17 yetu ikitolewa jasho na U17 ya Afrika Kusini pale Chamazi- wachezaji walionekana kabisa kulingana umri, lakini Amajimbos walituzidi kimchezo.
    Vijana wetu walionyesha wana vipaji pia, lakini walionekana kuzidiwa uzoefu na wenzao- tu kwa sababu Amajimbos wanacheza sana mashindano na vijana wetu hawaipati fursa hiyo.
    Ukweli ni kwamba tumepiga hatua katika dhana ya uwekezaji kwenye soka ya vijana kutoka enzi zile za kuchomekea vijeba- hadi sasa watoto halisi wamesheheni tayari kwa mashindano.
    Lakini tunahitaji sasa kufikiria namna ya kumuendeleza kijana baada ya kumuibua kwa kuhakikisha anacheza mashindano.
    Namna nzuri ambayo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kufanya kwa sasa chini ya rais wake, Jamal Malinzi ni kuhakikisha kunakuwa na ligi madhubuti ya vijana, vinginevyo timu zetu za taifa za vijana zitaendelea kuwa dhaifu mbele ya vijana wenzao walioiva. Ramadhani Karim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA KIASI FULANI, TUMEFANIKIWA KATIKA DHANA YA UWEKEZAJI KWENYE SOKA YA VIJANA, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top