• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2018

    MANJI ASIPORUDI MKUCHIKA ATAWAAMBIA NINI YANGA?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SINTOFAHAMU mpya imeibuka juu ya hatima ya uchaguzi wa Yanga baada ya jana kuonyeshwa na kusomwa barua ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji kurejea madarakani.
    Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga SC, Kapteni Mstaafu, George Huruma Mkuchika alisema kwamba ameandika barua ya kukubali kubaki katika nafasi ya Uenyekiti baada ya ombi, au zuio la wanachama.
    Na kwa sababu hiyo, Mkuchika amesema kwamba kufuatia tamko la kurejea kwa Manji, nafasi ya Uenyekiti haitajazwa katika uchaguzi ujao Januari 13, mwakani.

    Yussuf Manji (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa Yanga hivi karibuni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam

    Mkuchika aliionyesha na kuwasomea Waandishi wa Habari barua iliyoandikwa na Manji kujibu ombi la wanachama wa klabu hiyo kumtaka aendelee na nafasi hiyo kufuatia yeye mwenyewe kuandika barua ya kujiuzulu Mei mwaka jana baada ya miaka 11 akianza kama mfadhili mwaka 2006.
    Wanachama wa Yanga walikataa ombi la Manji kujiuzulu katika mkutano wa Juni 10, mwaka huu Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay mjini Dar es Salaam.
    “Kifupi anasema, nimepokea uamuzi wa wanachama wa Yanga, kwa bahati mbaya kipindi ninachoandikiwa mimi nipo kwenye matibabu, tarehe 15 Desemba madaktari wangu wanasema nitakuwa nimekamilika. Kwa hiyo pamoja na kwamba nimerudi kama Mwenyekiti, nitafanya kazi za kwenda ofisini kila mara kuanzia tarehe 15 Januari,”amesema Mkuchika akiisoma barua hiyo. 
    Mkuchika amesema Januari 15 Manji ataanza rasmi kazi za Yanga na kwenye makampuni yake baada ya kupitia kipindi kirefu cha misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka jana, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye kuwekwa rumande akidaiwa kumiliki pasipoti mbili na uhujumu uchumi, kesi ambazo zote zilifutwa.
    Kulingana na maelezo ya Mkuchika jana ni kwamba Manji atarejea Yanga SC Januari 15, yaani siku mbili baada ya uchaguzi Januari 13.
    Kwa kipindi chote hiki hatajihusisha na masuala ya klabu na hali iliyopo itaendelea kama ilivyo – klabu itaendelea kusafiri katika kipindi kigumu na siku ya uchaguzi Januari 13, wanachama watachagua Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne tu.
    Kana kwamba hiyo haitoshi, agizo la Serikali kutaka uchaguzi usimamiwe na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Yanga pia hawalitaki na Mkuchika jana alisema kufanya hivyo ni kuvunja katiba ya klabu yao.
    Kama uchaguzi utasimamiwa na Yanga wenyewe, kwa maana ya hao Wajumbe wanne waliobaki madarakani kati ya waliochaguliwa Juni mwaka 2016 kufuatia wengine wengi kujiuzulu nani ataamini utakuwa huru na wa haki?
    Ukiondoa Manji, wengine waliojiuzulu ni Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah na waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja ni wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Manji kama amerejea Yanga anapaswa kuonekana mwenyewe akizungumza na kuwaaminisha wana Yanga kwamba amerejea na si kusemewa au kusomwa kwa barua ambayo ni maandishi tu anayoweza kuandika na kusaini mtu yeyote ikadaiwa ni yeye.
    Na shaka zaidi ni pale inapoelezwa kwamba eti Manji ataanza kazi rasmi Januari 15, mwakani, yaani siku mbili baada ya uchaguzi – vipi asipoanza kazi baada ya uchaguzi na wanachama hawatachagua Mwenyekiti mpya Januari 13?
    Mkuchika ni mtu mwenye heshima kubwa sana katika taifa hili na si tu kwa klabu ya Yanga na anapaswa kufahamu kwamba suala limebeba hatima ya heshima yake mbele ya jamii. Kama kweli Manji atarejea itakuwa vizuri, na asiporudi Mkuchika atawaambia nini Yanga?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI ASIPORUDI MKUCHIKA ATAWAAMBIA NINI YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top