• HABARI MPYA

  Wednesday, October 03, 2018

  MO DEWJI AFANYA KWELI SIMBA SC, ‘MAGREDA’ YAANZA KAZI UJENZI WA UWANJA WA BUNJU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MMILIKI matarajiwa wa klabu ya Simba SC, Mohamed Gulam Dewji amesema kwamba zoezi la ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa klabu eneo la Bunju mjini Dar es Salaam limeanza.
  Mo Dewji ambaye yuko mbioni kununua asilimia 49 ya hisa za klabu, amesema kwamba anatarajia zoezi hilo lililoanza jana litakamilika kabla ya Februari 2 mwakani na ameposti picha ya Greda likisawazisha eneo la Uwanja wa Bunju.
  “Nimeanza kukamilisha ahadi ya uwanja wa Bunju. Insha'Allah kazi ya ujenzi itakamilika kabla ya mwezi wa 2, 2019. NguvuMoja," amesema Dewji.
  “Huu ni wakati wa kihistoria kwa klabu yetu. Kwa miaka mingi nimekuwa nikiota na sisi tuwe na Uwanja wetu wa mazoezi, na ninafurahi sasa ninawezesha hii ndoto baada ya miaka 82 tangu kuanzishwa kwa klabu yetu ya Simba,”.
  Mohamed Dewji amesema ameanza ujenzi wa Uwanja wa Bunju wa klabu ya Simba mjini Dar es Salaam 

  Katika mkutano uliofanyika Desemba 3, mwaka jana wanachama wa Simba  SC waliazimia kumfanya Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini kuwa mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
  Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
  Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI AFANYA KWELI SIMBA SC, ‘MAGREDA’ YAANZA KAZI UJENZI WA UWANJA WA BUNJU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top