• HABARI MPYA

  Tuesday, October 16, 2018

  KILA LA HERI TAIFA SARS, KAMA CAPE VERDE WALITUFUNGA KWAO NA SISI TUTAWAFUNGA KWETU LEO ‘INSHAALLAH’…AMIN

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inawakaribisha Cape Verde ‘Papa wa Bluu’ katika mchezo wa marudiano Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Taifa Stars watakuwa Uwanja wa nyumbani leo, siku tat utu wafungwe 3-0 na Papa wa Bluu Ijumaa katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa mjini Praia.
  Maana yake Taifa Stars inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kufufua matumaini ya kwenda AFCON ya mwakani nchini Cameroon.
  Kocha Mkuu, Mnigeria Emmanuel Amunike ambaye amemuongeza beki mkongwe Erasto Edward Nyoni kwenda kuziba pengo la beki wa kulia wa Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya jadi za njano anahitaji kubadili mbinu leo ili kupata ushindi.

  Baada ya kucheza kwa kujihami katika mechi mbili za ugenini Stars ikitoa sare ya 0-0 na Uganda Septemba 8 mjini Kampala na ile ya Ijumaa ikifungwa 3-0, leo atahitaji kutumia mfumo wa kushambulia.
  Pamoja na hayo, mabeki wa Taifa Stars watahitaji kuwa makini na mshambuliaji wa klabu ya Partizan ya Ligi Kuu ya Serbia, Ricardo Jorge Pires Gomes aliyefunga mabao mawili Ijumaa huku lingine likifungwa na beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares maarufu kama Stopira.
  Ikumbukwe Taifa Stars haijashinda mechi katika kundi lake hadi sasa baada ya sare ya 1-1 na Lesotho pia mwaka jana mjini Dar es Salaam.
  Uganda ambayo leo itakuwa ugenini kwa Lesotho ndiyo inaongoza Kundi L kwa sasa ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda mbili na kutoa sare, sasa ikifuatiwa na Cape Verde pointi nne za mechi tatu pia. Tanzania na Lesotho zinafuatia kila moja ikiwa na pointi mbili.
  Viingilio katika mechi ya leo itakayoonyeshwa moja kwa moja na ZBC 2 inayopatikana kwenye kisimbusi cha Azam TV ni Sh. 10,000 kwa majukwaa yote ya VIP yaani A, B na C wakati mzunguko itakuwa ni Sh. 2,000.
  Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Taifa Stars. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA SARS, KAMA CAPE VERDE WALITUFUNGA KWAO NA SISI TUTAWAFUNGA KWETU LEO ‘INSHAALLAH’…AMIN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top