• HABARI MPYA

    Monday, October 15, 2018

    FAMILIA YATOA OFA YA SH. BILIONI 1 KWA YEYOTE ATAKAYESAIDIA KUPATIKANA KWA BILIONEA MO DEWJI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    FAMILIA ya Mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji imetangaza zawadi ya Shilingi Bilioni 1 yeyote atakayesaidia kupatikana kwa mpendwa wao huyo, aliyetekwa Oktoba 11, mwaka huu.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika jengo la Golden Jubilee Towers ghorofa ya 20 mtaa wa Ohio, Posta mjini Dar es Salaam, baba mdogo wa M Dewji, Azim Dewji amesema kwamba fedha hizo zitatolewa kama zawadi kwa atakayesaidia kupatikana kwa mpendwa wao huyo.
    Dewji amesema kwamba Mwenye taarifa anaweza kuwasiliana na mwanafamilia, Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478, 0784783228 na email ya findmo@metl.net

    Donge nono la Sh. Bilioni 1 litatolewa kwa yeyote atakayesaidia kupatikana kwa Mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji 

    Dewji mwenye umri wa miaka 43 alitekwa Alhamisi asubuhi akiwa anaingia katika gym ya Collessium eneo la Masaki mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi baada ya watu wasiojulikana kufyatua risasi hewani mfululizo wakati bilionea huyo anateremka kwenye gari yake kabla ya kumbeba na kumpakia kwenye gari lao na kutokomea naye kwa kasi.
    Mohammed, mtoto wa mfanyabiashara wa siku nyingi, Gulamabbas Dewji – ni rais wa makampuni MeTL Group yaliyoasisiwa na baba yake huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM kati ya mwaka 2005 na 2015. 
    Februari mwaka huu ilielezwa utajiri wa Dewji unafikia dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hivyo kushika nafasi ya 17 katika orodha ya matajiri wa Afrika na kuwa mfanyabiashara kijana tajiri zaidi.
    Kwa sasa, Mo Dewji yuko mbioni kuwa mmiliki wa klabu ya Simba kufuatia mkutano wa wanachama wa Desemba 3, mwaka jana kuazimia kumfanya bilionea huyo kuwa mwanahisa mkuu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
    Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji. 
    Tayari Jeshi la Polisi limekwishawatia nguvuni watu zaidi ya 20 kwa ajili ya uchunguzi juu ya kutekwa kwa Bilionea huyo.
    Mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema kwamba Jeshi la Polisi nchini linaendelea kumtafuta mfayabiashara huyo likiwa na imani kubwa ya kumpata akiwa salama.
    Waziri Lugola amelitaka jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wake ili lisiwashikilie washukiwa kwa zaidi ya saa 24. Aidha, Waziri Lugola amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazoweza kulisaidia Jeshi la Polisi kupatikana kwa Mohammed Dewji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FAMILIA YATOA OFA YA SH. BILIONI 1 KWA YEYOTE ATAKAYESAIDIA KUPATIKANA KWA BILIONEA MO DEWJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top