• HABARI MPYA

  Sunday, January 01, 2017

  HATUWEZI KUJUA TUNAPOKWENDA, KAMA HATUJUI TULIPOTOKA

  HERI ya mwaka mpya. Naungana nanyi kumshukuru Mungu kwa kutuvusha salama kutoka 2016 hadi 2017.
  Na kumuomba Mwenye Mungu, aufanye mwaka 2017 uwe mzuri kwa ujumla kwetu, kama taifa na hata kwa mtu mmoja mmoja.
  Kwa baraka zake Mwenyezi Mungu tumeumaliza mwaka 2016 na leo tunauanza mwaka 2017. Tumeumaliza mwaka, ambao wengi wetu wanaamini ulikuwa mgumu hususan kiuchumi.
  Lakini katika sekta ya michezo, kwa ujumla tumeumaliza mwaka mwingine ambao hatukufanya vizuri.
  Jirani zetu Uganda jana wamekwenda Tunisia kuweka kambi ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Gabon wiki ijayo.
  Uganda wanarudi AFCON baada ya miaka 39 kufuatia uwekezaji na mkakati mzuri kwenye soka yao, uliowafanya wawe taifa lenye mafanikio zaidi miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
  Pamoja na mafanikio yao, Uganda wanayaweza yote katika mazingira magumu mno – hususan kifedha. Timu yao ya taifa, The Cranes inakwenda Tunisia kambini, huku kuna madai ya kocha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ kutolipwa mishahara kwa muda mrefu.
  The Cranes inakwenda kwenye kambi ya kujiandaa na AFCON huku kukiwa kuna taarifa kwamba hata posho za wachezaji zimekuwa ni tatizo.
  Uganda wanafanya yao katika mazingira magumu, lakini kwa sababu ya nidhamu na uzalendo wao wanayaweza na hatimaye wamerejea AFCON.
  Uganda wana Ligi madhubuti ambayo haijagubikwa na rushwa wala ushabiki uliokithiri hadi kwa viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi yao (FUFA), inayowasaidia kuzalisha wachezaji wazuri kila kukicha.
  Uganda wana Ligi na mashindano madhubuti ya vijana, yanayowasaidia kuibua na kukuza na vipaji. 
  Kuna wakati walianzisha hadi Ligi ya wachezaji wa akiba, kuwasaidia wachezaji ambao hawana nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao.
  Yaani Uganda wameenea mipango ya mpira kiasi kwamba huwezi kustaajabu mafanikio yao.
  Sisi kwetu tumeendelea kuwa waumini wa fitna, majungu na miujiza –  zaidi ni ushabiki wa kijinga kuanzia kwenye klabu, vyama na mashirikisho ya soka hadi kwenye vyombo vya habari.
  Katiba, Sheria na Kanuni zipo nchini lakini hata kama zinafanya kazi huwezi kuona zinafanya kazi, kwa sababu tumeweka mbele ushabiki.
  Mwaka 2016 wanachama wa klabu za Simba na Yanga walijaribu kupitisha mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kwa matarajio ya tofauti ya kimaendeleo pia, lakini wakakwamishwa na Serikali.
  Maana yake, tunauanza mwaka 2017 na Simba na Yanga zile zile za tangu miaka ya 1930 wakati zinaasisiwa huku tukiwa hatuna matarajio ya kama mpango wa mabadiliko utafanikiwa.
  Mwaka 2016 sisi wa vyombo vya habari tumetia fora kwa kusifia ujinga na kuzidi kuwajaza ujinga wapenzi wa michezo nchini, kiasi kwamba imefikia wakati wanaamini katika njia zisizo sahihi.
  Ni mambo ya kusikitisha na yote kwa pamoja yamechangia au yanachangia kuua soka yetu, iwe tunajua, au hatujui – lakini ni hivyo. 
  Mwaka 2016 Taifa limezidi kuporomoka katika sekta ya michezo na zaidi ya Yanga kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, au Mbwana Samatta kusajiliwa na KRC Genk ya Ubelgiji sijui tuna nini kingine cha kujivunia. 
  Ndiyo maana basi, wakati tunasherehekea kuumaliza mwaka 2016 na kuuanza mwaka 2017, vyema viongozi wa klabu, vyama na Mashirikisho ya michezo na sisi wa vyombo vya habari tukajitathmini pia kila mmoja kwa nafasi yake na wajibu wake katika ustawi wa sekta ya michezo nchini.
  Haitoshi kusherehekea mwaka mpya kwa kugongeshana glasi na kukumbatiana pasipo kujitathmini, maana ili ujue unapokwenda, lazima ujue unapotoka. Heri ya mwaka mpya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HATUWEZI KUJUA TUNAPOKWENDA, KAMA HATUJUI TULIPOTOKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top