• HABARI MPYA

    Sunday, January 29, 2017

    CHIRWA AIPANDISHA KILELENI YANGA, SIMBA WANAISOMA WAO SASA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa leo ametokea benchi na kufunga mabao yote, Yanga ikiilaza 2-0 Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo unaipandisha Yanga SC kileleni mwa Ligi Kuu ikifikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 20, ikiwashushia nafasi ya pili Simba SC waliojinafasi  kileleni kwa muda mrefu tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti mwaka jana.
    Chirwa alifunga mabao yote hayo kipindi cha pili baada ya kuingia kuchukua nafasi ya kiungo wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kipindi cha pili.
    Hiyo ilifuatia dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, timu hizo zikishambuliana kwa zamu, huku wageni wakionekana kuidhibiti kabisa Yanga.
    Obrey Chirwa (kulia) akiwa amembeba Simon Msuva kushangilia bao lake la kwanza jana. Kushoto ni Emmanuel Martin
    Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima akimruka kiungo wa Mwadui, Razack Khalfan
    Beki wa Mwadui, Iddi Mobby akimdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe
    Simon Msuva wa Yanga akimiliki mpira mbele ya Iddi Mobby wa Mwadui
    Deus Kaseke wa Yanga akipambana na Yassin Mustafa wa Mwadui FC

    Safu imara ya ulinzi ya Mwadui chini ya Iddi Mobby na Malika Ndeule iliwadhibiti washambuliaji hatari wa Yanga, Simon Msuva na Amissi Tambwe muda wote wa mchezo.
    Na kwa upande wa Yanga, mabeki wazoefu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan waliwadhibiti vizuri washambuliaji wa Mwadui, Awadh Juma na Paul Nonga.
    Hatimaye ukawadia wakati mzuri kwa Yanga kwenye mchezo huo kujipatia mabao yao mawili ndani ya dakika 13.
    Chirwa aliyesajiliwa msimu huu kutoka FC Platinums ya Zimbabwe, alifunga bao la kwanza dakika ya 69 kwa shuti kali akiuwahi mpira uliookolewa na kipa wa Mwadui FC, Shaaban Hassan Kado baada ya shuti la Simon Msuva.
    Bao hilo liliwapa furaha kubwa wapenzi wa Yanga, ambao kwa muda mrefu walikuwa wametulia wakifuatilia mchezo huo uliokuwa mkali kwa umakini.
    Na baada ya bao hilo, Mwadui wakajaribu kutoka kuelekeza mashambulizi langoni mwa Yanga kutafuta kusawazisha, lakini hiyo ikawagharimu kufungwa bao la pili.
    Alikuwa ni Chirwa, tena aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza baada ya wiki tatu za nje kwa maumivu, aliyefunga bao hilo dakika ya 82 kwa shuti baada ya kudondoshewa pasi ya kichwa na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kufuatia krosi ya beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi 'Dida', Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub 'Cannavaro', Justin Zulu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Said Juma ‘Makapu’ dk81, Haruna Niyonzima/Obrey Chirwa dk68 na Deus Kaseke/Emmanuel Martin dk52.
    Mwadui FC; Shaaban Kado, Nassor Masoud 'Chollo', Malika Ndeule, Yassin Mustafa/David Luhende dk81, Iddi Mobby, Razack Khalfan, Hassan Kabunda/Salum Kanoni dk89, Awadh Juma, Paul Nonga, Salim Khamis/Joseph Kimwaga dk86 na Abdallah Seseme.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHIRWA AIPANDISHA KILELENI YANGA, SIMBA WANAISOMA WAO SASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top