• HABARI MPYA

    Tuesday, January 31, 2017

    SIMBA NAO WAKATAA KUCHEZA NA MAMELODI KESHO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC nayo imegoma kucheza na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mchezo ambao ulitarajiwa kufanyika kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Meneja wa Simba, Mussa Hassan Mgosi amesema leo kwamba Kocha Mkuu, Joseph Omog amewasilisha mapendekezo yake kwa uongozi kwamba hawezi kucheza mechi hiyo.
    Mgosi amesema sababu ziko wazi kwamba kwa sasa Simba SC ipo kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inagombania pointi za kutafuta ubingwa, hivyo haiwezi kujihusisha na kitu kingine.
    “Kwa mfano kwa sasa tuna mechi na Maji Maji mjini Songea Jumamosi, unataka tucheze mechi na Mamelodi Jumatano, maana yake Alhamisi ndiyo tuondoke Dar es Salaam kwenda Songea. Tufike kule usiku, Ijumaa tufanye mazoezi, Jumamosi tucheze mechi. Kwanza tutachoka, lakini pili ikitokea mtu akaumia kwenye mechi na Mamelodi itakuwaje?”alihoji Mgosi.
    Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, alisema mchezo huo ulikuwa mzuri na muhimu kwao, lakini kutokana na tu umekuja katika wakati mbaya wanalazimika kuuacha.
    Simba wanaungana na watani wao wa jadi, Yanga kugoma na kucheza na Mamelodi na sasa mabingwa hao wa Afrika Kusini watamenyana na Azam FC tu kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Awali ilipangwa Mamelodi icheze na Simba Jumatano na Ijumaa icheze na Yanga, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Jana Yanga walikuwa wa kwanza kukataa kucheza na mabingwa hao wa Afrika, Mamelodi kwa sababu kocha wao, Mzambia George Lwandamina alikataa kwa kuwa mechi inaingilia programu zake.
    Timu hiyo maarufu kama ‘Wabrazil’ kutokana na kuvalia jezi za njano kama timu ya taifa ya Brazil, iliwasili jana nchini na inakuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam.
    Mkurugenzi wa African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamuda’ alisema Mamelodi wanakuja nchini kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili, iitwayo Linda Tembo Wetu.  
    Timu hiyo ya bilionea wa madini Afrika Kusini, Patrice Motsepe kwa hapa nchini kwenye mechi za mashindano imewahi kucheza Yanga SC pekee katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001.
    Ilikuwa ni katika hatua ya 16 Bora kwenye Ligi ya Mabingwa na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 6-5 baada ya kufungwa 3-2 Pretoria Mei 13 na kulazimishwa sare ya 3-3 Mei 26 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NAO WAKATAA KUCHEZA NA MAMELODI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top