• HABARI MPYA

    Tuesday, January 24, 2017

    WANAOSHINDWA KUPANGA RATIBA, WATAWEZA KUTENGENEZA PROGRAMU ZA MAENDELEO?

    Na Haji Manara, DAR ES SALAAM  
    KUNA kulogwa na kujiloga. Kuna kufa na kujiua pia kulia na kuliliwa. Sisi Watanzania hakika tupo katika fungu la pili, fungu la kukosa, fungu mzigo, tunajiloga, tunajiua na tunaliliwa.
    Hakika hatujui twataka nini, hatujui malengo yetu, lakini kubwa hatujui hata tutokapo wala tuendako, na leo naandika kitu kidogo tu kinachotushinda kwenye soka letu, RATIBA.
    Wakati wenzetu wanazungumzia changamoto nzito na kubwa katika maendeleo yao ya mchezo murua zaidi duniani wa soka, Watanzania tunahangaika namna ya kupanga ratiba ya mechi za mashindano yetu ya nyumbani za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Ratiba inayobadilishwa Kama nguo, tena mvaaji mwenyewe ni mbunifu wa mavazi au mwanamitindo, ambaye huvaa nguo tano kwa siku.
    Siku za nyuma niliwahi kusema kwamba, iwapo ratiba ya Ligi Kuu nchini haitapanguliwa baada ya kupangwa, nitatembea bila shati kutoka Mtaa Msimbazi hadi zilipo ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.
    Nilidhani Kwa kusena vile walau TFF na bodi ya Ligi wataona haya na kuhakikisha ratiba ya Ligi Kuu haibadilishwi tena, kumbe ndio kwanza wakubwa wameweka gundi masikioni, tangu wakati ule ratiba imekwishafumuliwa mara tatu, na leo hii imebadilishwa tena, Kwa kisinguzio kile kile, eti ratiba za CAF na za ligi zimeingiliana. 
    Ninajiuliza iwapo ratiba ya Ligi yetu ni muhali kuipanga,vipi kuhusu programu nyingine za maendeleo? 
    Itakuwaje kuhusu timu yetu ya taifa juu ya ndoto zetu za mchana wa jua kali? vipi kuhusiana na zile programu hewa za soka la vijana, watoto na wanawake?
    Hakika kwetu hayo ni sawa na bahari ya Mediterranean au bahari kuu ya hadithi za Alfu Leila uleila, hatuwezi ratiba tutaweza kwenda Afcon 2019? hatuwezi kupanga ratiba tutaweza kuwa na mipango madhubuti ya kuendeleza mchezo huu ambao yatajwa watu bilioni tatu duniani kote wanaushabikia? 
    Kama tumerogwa aliyeturoga Kafa, hatuponi hadi Kiyama , tutakapokutana nae mchawi wetu. 
    Nimalizie Kwa kuwapa mtihani mwingine TFF na bodi ya Ligi, iwapo Kama ratiba yao ya Ligi kuu na Kombe la shirikisho haitabadilishwa kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu, ntamposa mlimbwende Wema Sepetu, na akikubali ntamuoa, akikataa ntatembea na boxer toka Nyumbani kwangu hadi TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANAOSHINDWA KUPANGA RATIBA, WATAWEZA KUTENGENEZA PROGRAMU ZA MAENDELEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top