• HABARI MPYA

    Monday, January 30, 2017

    SERIKALI YAUNGA MKONO PROGRAMU YA TFF OLIMPIKI 2020

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kwamba inaunga mkono juhudi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika programu za maendeleo ya vijana, hususani nia yake ya dhati kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan mwaka 2020.
    Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari ndiye aliyesema hayo mara baada ya kusikia program za TFF kutoka kwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau katika hafla ya uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki.
    “Nimesikia program mbalimbali za TFF, naona zinakuja wakati mwafaka. Nimewapongeze kwa mipango yenu mizuri kwa sababu inaleta matumaini. Jambo kubwa ambalo linanisukuma na kuwapongeza ni kuwa na program ya vijana, hatuwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na program ya vijana.
    “Serikali inatambua haya yote mnayofanya. Na ili kuboresha, Serikali imetenga shule 55 ambazo zitakuwa ni maalumu kwa ajili ya vijana, lengo ni kupata vipaji bora ambavyo vitakuwa vikiendelezwa, huku wakiwa wanapata elimu.
    “Watanzania wana kiu kubwa ya mafanikio, lakini tunafikaje katika katika safari hii tunayoianza leo? Tutafika tu, iwapo kutakuwa na ushirikiano licha ya kutoangalia aina ya usafiri ambao tutatumia,” alisema Singo huku wadau wa mpira wa miguu wakimsikiliza kwa makini.
    Aliendelea, “Nasikia mmeunda Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu hususani vijana. Ni jambo zuri, lakini rai yangu ni kwamba watakaunda kamati ya mfuko huo wawe watu respected ili wananchi waipende na ikiwa hivyo itafanikiwa. Sisi Serikali tutafanya kazi bega kwa bega na kamati hiyo. Jambo kubwa, ni kwamba lazima tukutane mara kwa mara.”
    Kabla ya Mkurugenzi Singo kuzungumza, Makamu Rais wa TOC, Ndugu Tandau, alipongeza pia harakati za kuanza mapema akisema: “Shukrani TFF kwa kuthamini TOC. Ni vizuri tumeanza mapema. Michuano ya Olimipiki ni mikubwa na inahitaji timu zenye viwango vya juu kufanikiwa kufuzu.”
    Alieleza hadhara iliyohudhuria hafla hiyo, kuwa TOC inakuwa na Mawasiliano ya maandalizi Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki inayoitwa ‘Olympic Solidarity Program’ ambayo hutoa sehemu ya fungu ya maandalizi na kwamba TFF haina budi kuwasilisha program yake kwa ajili ya kuingia kwenye bajeti ambayo inaitwa ‘Team Support Grant’.
    “Sasa tuwe kitu kimoja toka huu mwanzo na mambo yaende kwa uwazo na kupeana taarifa kila wakati,” alisema Tandau.
    Awali kabla ya viongozi hao kuzungumza, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kinachofanywa sasa na Shirikisho si kutafuta miujiza kwenye matokeo badala yake ni kujenga timu (Maandalizi) kwa dhana kwamba “Timu za Taifa haziokotwi kama embe dodo.”
    “Mhe. Mkurugenzi, kujenga timu hizi ni gharama kubwa. Hata matunda ambayo tunasubiri moshi mweupe ya timu ya vijana, hayakutokea hivi hivi ni maandalizi. Si ajabu kabla ya mwisho wa wiki hii tukaona moshi mweupe,” alisema Malinzi.
    Alisema ili vijana wa Tanzania waweze kufanya vema, hakuna budi wadau wakiwamo Serikali, Kampuni, Mashirika ya umma na watu binafasi kusapoti mbio hizo za kwenda Tokyo, Japan pamoja na timu nyingine za taifa. “Program nzima ni gharama kubwa,”
    Kadhalika, ili kutekeleza program hiyo, Rais Malinzi alizungumzia utulivu katika kufanya kazi kwa sasa kwa kuwa historia inaonesha kuwa kumekuwa na nia ovu ya baadhi ya wadau kutaka kutibua mambo mazuri yanayofanywa na uongozi wa mpira wa miguu.
    “Naomba tuelekeze mafanikio yetu kwa kushirikiana na kuutendea haki mpira wa miguu kwa kushirikiana kwa sababu soka ni furaha na ili kufanikiwa linahitaji juhudi za pamoja,” alisema Malinzi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAUNGA MKONO PROGRAMU YA TFF OLIMPIKI 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top