• HABARI MPYA

    Saturday, January 28, 2017

    AZAM YAICHAPA SIMBA TENA 1-0, SAFARI HII NI BOCCO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAO pekee la Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ limetosha kuipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bocco alifunga bao hilo dakika ya 70 baada ya makosa ya beki Mzimbabwe, Method Mwanjali kutaka ‘kuuremba’ mpira kwenye eneo la hatari naye akaupitia na kwenda kumchambua kipa Mghana, Daniel Agyei.   
    Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo ndani ya mwezi mmoja Simba wanapewa na Azam, baada ya Januari 13 kufungwa pia 1-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao pekee la Himid Mao. 
    John Bocco (kulia) akimlamba chenga beki wa Simba, Method Mwanjali leo
    Kipa wa Azam, Aishi Manula akidaka mpira dhidi ya kiungo wa Simba, Jamal Mnyate huku mchezaji mwenzake, Joseph Mahundi akiwa tayari kusaidia
    Kiungo wa Simba, Muzamil Yassin akipasua katikati ya wachezaji wa Azam, Joseph Mahundi (kushoto) na Frank Domayo (kulia)
    Mshambuliaji wa Simba, Juma Luizio akijaribu kupasua katikati ya mabeki wa Azam, Mghana Yakubu Mohamed (kushoto) na Gardiel Michael (kulia)

    Kipigo hicho kinapunguza matumaini ya ubingwa kwa Simba SC, iliyouanza vizuri msimu, kwani ikibaki na pointi zake 45 za baada ya kucheza mechi 20 inaweza kuenguliwa kileleni na Yanga ikiifunga Mwadui Uwanja wa Taifa.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka aliyesaidiwa na washika vibendera Hassan Zani, wote wa Arusha na Josephat Masija wa Mwanza, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilishuhudiwa timu zote zikicheza kwa kujihami zaidi.
    Makocha wote Mcameroon Joseph Marius Omog na Mromania Aristica Cioaba walianzisha mshambuliaji mmoja mmoja katika vikosi vyao, upande wa Azam Nahodha John Bocco na Simba, Juma Luizio.
    Kulikuwa na viungo wengi kwa timu zote, upande wa Azam wakianzishwa, Mcameroon Stephan Kingue, Himid Mao, Joseph Mahundi, Frank Domayo na Ramadhani Singano ‘Messi’ na Simba wakianzishwa Jonas Mkude, Said Ndemla, Jamal Mnyate, Muzamil Yassin na Pastory Athanas.
    Kwa sababu hiyo haikuwa ajabu timu zote kumaliza dakika 45 zikiwa zimemiliki sawa mpira, ingawa tu hakukuwa na mashambulizi ya kusisimua.
    Kipindi cha pili, makocha wote wakaamua kufunguka kwa kuingiza washambuliaji zaidi wakitoa mabeki na viungo. 
    Mabadiliko hayo yalifanya mchezo uanze kuwa mtamu kutokana na kushambuliana kwa zamu.
    Hata hivyo, ilikuwa ni bahati yao Azam FC baada ya kosa kosa za pande zote mbili kwa muda mrefu, Nahodha Bocco akafunga dakika ya 70.
    Bocco mwenye bahati ya kufunga dhidi ya vigogo Simba na Yanga, alifunga bao hilo pekee dakika ya 70.
    Baada ya kuruhusu bao hilo, Simba wakafunguka zaidi kusaka bao la kusawazisha kwa kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Azam.
    Lakini safu ya ulinzi ya Azam ikiongozwa na ‘beki mbabe’, Aggrey Morris ilisimama imara kudhibiti mashambulizi yote ya Simba.
    Kikodi cha Simba SC leo kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokungu/Ibrahim Hajib dk59, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Said Ndemla, Jamal Mnyate/Shiza Kichuya dk47, Muzamil Yassin, Pastory Athanas na Juma Luizio/Laudit Mavugo dk65.
    Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Mudathir Yahya dk77, Himid Mao, Joseph Mahundi, Frank Domayo, John Bocco/Abdallah Kheri dk83 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Yahya Mohammed dk63.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAICHAPA SIMBA TENA 1-0, SAFARI HII NI BOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top