• HABARI MPYA

    Sunday, February 14, 2016

    YANGA SC WAKIRUDIA TENA ‘KUCHEZEA SHILINGI CHOONI’, ITAKULA KWAO!

    WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC jana wameanza vizuri baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim nchini Mauritius katika mchezo wa kwanza Raundi ya Awali.
    Shukrani kwake, mfungaji wa bao hilo pekee, katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe, Mauritius, Mzimbabwe Donald Ngoma.
    Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa watakuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam, wakihitaji hata sare ili kusonga mbele, ambako watakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.

    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hubert Marie Bruno Andriamiharisoa, Randrianarivelo Ravonirina Harizo na Augustin Gabriel Herinirina, Ngoma alifunga bao hilo dakika ya 17 tu akimalizia krosi maridadi ya beki wa kulia, Juma Abdul Jaffar. 
    Pamoja na ushindi huo, Watanzania wengi wakiwemo mashabiki wa Yanga SC wenyewe hawakuwa na imani kama timu hiyo ingewea kupata matokeo mazuri jana, licha ya dhana iliyokuwapo kwamba imepangwa na timu dhaifu.
    Hiyo inatokana na kuchelewa kuondoka nchini na kujikuta wanawasili Mauritius usiku wa manane siku ya kuamkia mchezo ambao ulichezwa mchana.
    Kwa mujibu wa Yanga SC wenyewe, sababu za kuchelewa kufika Mauritius ni awali kukosa ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, Afrika Kusini kwenda Curepipe iwapo wangetumia ndege ya shirika la Ndege la Afrika Kusini (S.A.).
    Ikumbukwe, awali Yanga SC walipanga kuondoka Jumatano wiki hii na ndege ya S.A., ambayo ilikuwa siku mwafaka, kwa sababu wangefika mapema na kupata muda mzuri wa kuzoea hali ya hewa ya huko.
    Lakini Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Jerry Muro akasema S.A. iliwapa ratiba ya kushinda karibu kutwa nzima baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa O Tambo, Johannesburg kabla ya kuunganisha ndege ya Curepipe.
    Hivyo Yanga SC hiyo wakaona hiyo itawachosha wachezaji wao na wakaahirisha safari hadi Ijumaa Alfajiri kwa mujibu wa maelezo ya Jerry Muro.
    Hata hivyo, kufika Ijumaa Yanga SC walishinda kutwa nzima Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kabla ya kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) Saa 1:00 usiku na kuondoka nusu saa baadaye.
    Sababu zilizoelezwa na Yanga SC wenyewe za kushinda JNIA ni kwamba eti ndege ya ATC waliotarajia kusafiri nayo ilikuwa ina hitilafu, hivyo ilikuwa inarekebishwa.
    Inawezekana, ndiyo maana timu iliwasili JNIA, lakini wachezaji wakasoteshwa Uwanja wa ndege hadi usiku walipoondoka.
    Kwa kawaida unapokwenda kwenye mchezo wa ugenini, unapaswa kufika japo siku moja kabla – kwanza ajili ya kushiriki kikao cha kabla ya mechi siku moja kabla na pia kupata fursa ya kufanya mazoezi katika Uwanja ambao utatumika kwa mchezo.
    Ni muhimu kuujua Uwanja unaokwenda kuutumia kabla ya mchezo – na ndiyo maana Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likaweka sheria hiyo.
    Lakini Yanga SC walipoteza fursa hiyo kutokana na kuchelewa, kwa sababu ambazo wamezielewa wenyewe.
    Bila shaka, wakati wanasota kutwa nzima Uwanja wa Ndege wa Dar Ijumaa, Yanga SC walijuta kuacha kuondoka na ndege ya S.A. ambayo wangekaa Uwanja wa Ndege wa O Tambo kwa saa nne kabla ya kuunganisha ndege ya Curepipe.
    Ndiyo, ilifikia wakati hiyo ikawa ndiyo nafuu – lakini mabadiliko yoyote yasingeweza kufanyika ndani ya muda ule.
    Wamshukuru Mungu wameshinda mchezo wa jana na akili zao zimehamia kwenye mchezo dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC Jumamosi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Lakini ukweli ni kwamba Yanga SC jana ‘ilichezea shilingi chooni’ na lolote lingeweza kutokea na kusingekuwa na mwingine yeyote wa kulaumiwa, zaidi ya viongozi wenyewe wa klabu hiyo.
    Ndege si kama mabasi ya Ubungo, ratiba zake zinajulikana hata mwezi mmoja kabla – Yanga SC walipaswa kujipanga mapema kwa safari yao ya Mauritius kuepuka hali iliyotokea.
    Yanga SC wanapaswa kubadilisha utaratibu wao na kuhakikisha japo wiki mbili kabla wanakuwa wamekamilisha utaratibu kwa safari za nje.  
    Soka ya sasa imebadilika na hakuna timu ndogo tena – siku hizi timu zote zinaheshimu wapinzani zinaopangiwa katika mashindano.
    Miaka ya nyuma ilikuwa inafahamika wazi, Yanga SC inapokutana na timu za Kaskazini mwa Afrika inakwenda kupigwa mabao mengi, lakini sasa si hivyo tena na hayo ndiyo mabadiliko yenyewe kwenye mchezo.
    Kama Yanga SC waliidharau Cercle de Joachim, walifanya makosa na hawapaswi kuidharau tena hata kuelekea kwenye mchezo wa marudiano Dar es Salaam wiki mbili zijazo. Bin Zubeiry hapa! Wasalaam.      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAKIRUDIA TENA ‘KUCHEZEA SHILINGI CHOONI’, ITAKULA KWAO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top