• HABARI MPYA

    Saturday, February 13, 2016

    KIIZA AIPAISHA KILELENI SIMBA SC…NA SASA NDIYE MFALME WA MABAO VPL

    Na Princess Asia, SHINYANGA
    MABAO mawili ya mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza yametosha kuipa Simba SC ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inapanda kileleni mwa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ikifikisha pointi 45, baada ya kucheza mechi 19, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi. 
    Hamisi Kiiza (kulia) akifurahia na Ibrahim Hajib baada ya kufunga leo mjini Shinyanga


    Aidha, Simba SC watalazimika kuiombea ‘dua mbaya’ Azam FC katika mchezo wake wa kesho dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iendelee kubaki kileleni.
    Azam FC itaingia kumenyana na Coastal kesho, ikiwa na pointi 42 – maana yake wakishinda kwa wastani mzuri wa mabao watarejea kileleni.  
    Kiiza alifunga mabao yake katika dakika za 34 na 47, hivyo sasa anaongoza kwa kufunga Ligi Kuu akifikisha mabao 16 dhidi ya 14, ya mshambuliaji wa mahasimu, Yanga SC, Mrundi Amissi Tambwe.
    Stand United ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa David Ossuman. Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, African Sports imeifunga 1-0 Mgambo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati kocha Mmalawi, Kinnah Phiri ameanza na ushindi wa 5-1 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Sokoine, Mbeya. 
    Mabao ya MCC yamefungwa na Raphael Alfa kwa penalti dakika ya tano, baada kiungo mshambuliaji wa Mbeya City Ditrim Nchimbi kuchezewa vibaya kwenye boksi, Ramadhani Chombo 'Redondo' dakika ya 35, Haruna Moshi 'Boban', dakika ya 41 na 43 na Meshack Samueli dakika ya 79, wakati bao pekee la Toto lilifungwa na Japhet Mkala dakika ya 78.
    Ndanda FC imeifunga 1-0 Majimaji Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, wakati JKT Ruvu imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy/Mussa Mgosi dk86, Emery Nimubona, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Brain Majwega dk50, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu/Danny Lyanga dk66 na Said Ndemla.
    Stand United: Frank Muwonge, Revocatus Richard, Seleman Mrisho, Nassor Masoud, David Ossuman, Jacob Masawe, Pastory Athanas, Amri Kiemba, Seleman Selembe/Jeremiah Katura dk49, Hassan Banda/Elias Maguli dk49 na Vitalis Mayanga/Fred Hamisi dk75.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIIZA AIPAISHA KILELENI SIMBA SC…NA SASA NDIYE MFALME WA MABAO VPL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top