• HABARI MPYA

    Monday, November 23, 2015

    KAVUMBANGU: NAWASIKIA SIKIA TU SIMBA SC, LAKINI SIWAELEWI!

    Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
    MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Didier Kavumbangu amesema amekuwa akisikia sikia tu habari za kutakiwa na Simba SC, lakini hajawahi kuzungumza na kiongozi yeyote wa klabu hiyo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE mjini Addis Ababa, Ethiopia mwishoni mwa wiki, Kavumbangu amesema kwamba na wala klabu yake, Azam FC haijawahi kumpa taarifa zozote za kuhamishwa kwa mkopo.
    “Nasikia Simba SC wananitaka kwa mkopo. Nasikia sikia tu, lakini sijawahi kuambiwa na klabu yangu, wala Simba SC hawajawahi kunifuata,”amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC na TP Mazembe ya DRC.
    Didier Kavumbangu amesema kwamba anasikia Simba SC wanamtaka, lakini hawajawahi kuzungumza naye

    Alipoulizwa iwapo Simba SC wana nia kweli ya kumchukua, Kavumbangu anayechezea Burundi kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge amesema; “Siwezi kuzungumza hadi Simba wakinifuata ndiyo nitawajibu, lakini kwa sasa mimi ni mchezaji wa Azam FC na nina Mkataba,”amesema.
    Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva mwishoni mwa wiki alisema kwamba hawajawahi kufanya mazungumzo na Kavumbangu, lakini wanasikia nao kwamba Azam FC inataka kumuacha.
    “Kwa sasa hatuwezi kuzungumza chochote, hadi hao Azam FC wamuache, labda tunaweza kuzungumza, tunakiri ni mchezaji mzuri,”alisema.
    Kavumbangu alijiunga na Azam FC msimu uliopita kutoka Yanga SC na alikuwa na msimu mzuri wa kwanza chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akicheza na kufunga mabao, kiasi cha kuwafurahisha hadi wamiliki wa timu, akaongezwa Mkataba wa mwaka mmoja.
    Hata hivyo, baada ya kurejeshwa kwa Muingereza Stewart John Hall, Kavumbangu amepoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake.
    Lakini mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kavumbangu alianzishwa zote na akafunga katika kilamechi na kutimiza jumla ya mabao 19 ya kufunga katika mechi 46 za mashindano yote alizocheza. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAVUMBANGU: NAWASIKIA SIKIA TU SIMBA SC, LAKINI SIWAELEWI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top