• HABARI MPYA

    Wednesday, November 18, 2015

    BRAZIL WALIPIGWA 7-1 NA UJERUMANI NYUMBANI, AJABU GANI STARS!

    JULAI 8, mwaka 2014 wenyeji Brazil walifungwa mabao 7-1 na Ujerumani katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Dunia Uwanja wa Mineirao mjini Belo Horizonte.
    Ni kipigo kilichowaumiza Wabrazil, hususan wakizingatia wamefungwa kwenye ardhi ya nyumbani – lakini baada ya hapo, walijipanga upya na sasa wako vizuri tena.
    Brazil wako imara tena na watu wote wa Brazil wamesahau hayo ya kufungwa saba na Wajerumani.
    Kipigo kama hicho wamepata Tanzania jana mbele ya wenyeji Algeria na kutolewa katika mbio za kugombania tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi, baada ya kufungwa mabao 7-0 Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida.

    Matokeo hayo, yanaifanya Taifa Stars itolewe kwa jumla ya mabao 9-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 na Mbweha hao wa Jangwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi mjini Dar es Salaam.
    Hali ilikuwa mbaya kwa Taifa Stars jana, baada ya kuruhusu bao la kwanza mapema tu sekunde ya 43 dakika ya kwanza, mfungaji Yacine Brahimi.
    Himid Mao alipokonywa mpira katikati ya Uwanja na Mesloub Walid ambaye alipitia upande wa kushoto kwa Mwinyi Hajji Mngwali, kabla ya kutia krosi iliyounganishwa nyavuni na Brahimi.
    Hakika bao hilo liliwaondoa mno mchezoni Taifa Stars walioingia na hesabu za kupata wao bao la mapema – hivyo kujikuta wakipoteana uwanjani.
    Na Algeria walikuwa wakicheza kwa kasi mno wanapokuwa kwenye nusu ya wapinzani, ambao hawakuwa na wachezaji wa kutosha wa kuwadhibiti.
    Taifa Stars jana kwa kutaka kushambulia zaidi, ilitumia viungo wawili na washambuliaji watatu, wakati pia ilikuwa na kiungo mmoja wa pembeni.
    Farid Mussa aliyecheza pembeni juu, alikuwa tu anashuka kumsaidia Shomary Kapombe, lakini ukweli ni kwamba eneo la katikati Stars walizidiwa. 
    Algeria walipata bao la pili dakika ya 23 kupitia kwa Ghoulam Faouzi aliyepiga shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa zaidi ya 20, baada ya kiungo Mudathir Yahya kumchezea rafu Mesloub Walid na kuonyeshwa kadi ya njano.
    Mshambuliaji Elias Maguri aliifungia Taifa Stars bao dakika ya 27 kwa shuti la mbali nje ya boki, lakini pamoja na refa Alioum Alioum kuelekea kukubali, akaghairi baada ya ushauri wa msaidizi wake namba mbili, Noupue Nguegoue.
    Mudathir Yahya alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 40 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 40 kwa kumkwatua Yacine Brahimi
    Na Mahrez Ryad akaifungia Algeria bao la tatu dakika ya 41 kwa shuti kali, akimalizia krosi ya Islam Slimani.
    Kipindi cha pili, kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko akiwatoa kipa Ally Mustafa Barthez na winga Farid Mussa na kuwiangiza kipa Aishi Manula na kiungo Salum Telela.
    Mabadiliko hayo hayakuwa na msaada wowote kwa Taifa Stars, kwani Algeria ilinufaika zaidi kipindi cha pili kwa kupata mabao manne zaidi.   
    Islam Slimani alifunga bao la nne dakika ya 48 kwa penalti baada ya Mahrez kugongana na beki wa Taifa Stars, Kevin Yondan.
    Ghezzal Faouzi akafunga bao la tano dakika ya 58 kwa penalti baada ya Slimani kugongana na Aishi Manula kwenye boksi wakigombea mpira.
    Nahodha wa Mbweha wa Jangwani, Carl Medjani akafunga bao la sita kwa kichwa akimalizia kona ya Mahrez.
    Ghezzal Rachid aliyetokea benchi akafunga bao la saba dakika ya 74 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa Mahrez.
    Taifa Stars ikazinduka baada ya bao hilo na kukaribia kufunga mara mbili, kupitia kwa washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.  
    Dakika ya 85 Ulimwengu alimpa pasi nzuri Samatta baada ya wawili hao kugongeana vizuri, lakini Mbwana akapiga nje.
    Na dakika ya 89, Maguri alimpa pasi nzuri Ulimwengu akafanikiwa kumtoka beki Carl Medjani, lakini kipa M’bolhi Rais akaugusa mpira kidogo na kutoka nje, ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
    Kipigo hicho hakika kimewaumiza wachezaji, benchi la ufundi na zaidi Samatta ambaye ameingia kwenye 10 Bora ya kuwania tuo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
    Baada ya mafanikio ya kuiwezesha TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika, Samatta alitamani kufanya vizuri katika mchezo huo wa kufuzu Kombe la Dunia.
    Hata kama kutolewa, lakini si kwa kipigo cha aina ile – alionekana kama aliyekata tamaa, lakini bado na ana nafasi ya kushinda tuzo hiyo kwa sababu inaonekana ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi katika mashindano ya Afrika.
    Kombe la Dunia ni mashindano ya FIFA yanayokutanisha na wachezaji wanaocheza Ulaya na nchi nyingine zote duniani- lakini Ligi ya Mabuingwa Afrika ni ya Waafrika tu.
    Sahau kuhusu Samatta. Vipi mustakabali wa Taifa Stars baada ya kipigo cha jana? Tumeona Wabrazil walijipanga upya baada ya kipigo cha Julai 8 mwaka jana kutoka kwa Ujerumani.
    Ni kweli walimfukuza kocha Luis Fillipe Scolari na kumrejesha Carlos Dunga, lakini wachezaji wameendelea kuwa wale wale na timu inafanya vizuri.
    Labda Brazil walikuwa wa sababu ya kumfukuza kocha – ingawa mapema tu mimi sikuiona zaidi ya kumtoa kafara.
    Charles Boniface Mkwasa ni kocha aliyeanza kazi Agosti mwaka huu baada ya mwendo mbaya wa timu chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij.
    Na kazi yake kwa kweli imeonekana ndani ya muda mfupi – tu anahitaji muda zaidi kuendelea kutengeneza timu, kwa sababu kuna wachezaji wanakosekana kwa sasa katika timu na hatuna kabisa nchini.
    Hiyo siyo sababu ya kufungwa na Algeria, bali kuzidiwa uwezo na mbinu za kimchezo ndiyo leo zinatuondoa mapema katika mbio za Kombe la Dunia 2018.
    Wazi hiki ni kipindi kigumu kwa wachezaji wa Taifa Stars, makocha na hata viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya matokeo ya jana.
    Watazomewa na kushambuliwa na vyombo vya habari – wanaojiita wachambuzi nchini, watasahau kuelezea sababu za kimchezo za Stars kufungwa jana, watatuambia; “Hatuna msingi” na mengine mengi ya kukatisha tamaa.
    Lakini ukweli ni kwamba Taifa Stars jana ilifungwa kimchezo kabisa kama ambavyo Brazil walifungwa na Ujerumani mwaka jana nyumbani kwao katika Kombe la Dunia.
    Baada ya sare ya 2-2 nyumbani, Mkwasa na washirika wake, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ walitamani kwenda kushambulia zaidi na ugenini katika Uwanja ambao ulikuwa unamwagiwa maji ili uteleze na wachezaji wetu hawakuwa na viatu vya kucheza kwenye eneo la aina hilo.
    Mimi si muumini wa sababu za baada ya matokeo ya mabaya, ambazo mwisho wa siku huwa ni visingizio tu, bali nachoamini tumefungwa kimchezo na huo siyo mwisho wa dunia.
    Baadaye tutarudi kwenye ratiba za mashindano mengine ya kimataifa – na ninachokiona kwa sasa TFF ielekeze hasira zake kwenye ule mpango mkakati wake wa kuhakikisha kila wakati tunakuwa na wachezaji bora kwa kuwekeza kwenye soka ya vijana.
    Brazil walikuwa wana msingi imara, tena wa miaka mingi, lakini walifungwa saba na Ujerumani, sembuse sisi ambao kila siku ‘wachambuzi’ wanasema hatuna msingi? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BRAZIL WALIPIGWA 7-1 NA UJERUMANI NYUMBANI, AJABU GANI STARS! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top