• HABARI MPYA

    Saturday, November 28, 2015

    MWETA: KIPA WA SIMBA, MDOGO WA DUDU BAYA ALIYEANZISHA ‘AKADEMI’

    Na Princess Asia, MTWARA
    KIPA wa zamani wa Simba SC, Wilbert ‘Willy’ Mweta William ameanzisha kituo cha soka, kiitwacho Mweta Sports Center.
    Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE wiki hii, Mweta amesema kwamba kituo hicho kilianza mwaka 2013 kabla ya kusajiliwa rasmi Januari 22, mwaka 2015.
    Mweta Sports Center ipo Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza na ina watoto 86 wa kuanzia umri wa chini ya miaka 12 hadi hadi chini ya miaka 17.
    Mweta anasema kituo kina makocha watatu ambao ni John Bunguba, Emmanuel Thobias na Mataluma Charles Mataluma na kwamba anaendesha kituo hicho kutokana na mshahara wake katika klabu ya Ndanda FC ya Mtwara anayochezea kwa sasa.
    “Zaidi ya hapo kuna wadau mbalimbali wanaojua umuhimu wa hili jambo, wananipa sapoti kidogo. Namshukuru Mungu tunaendelea vizuri. Hakuna tatizo,”anasema.
    Wilbert 'Willy' Mweta enzi zake akidakia klabua ya Simba SC ya Dar es Salaam

    WILLY MWETA NI NANI?
    Albert Mweta alizaliwa Julai 1, mwaka 1988 Kisesa mkoani Mwanza na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Kanyama kabla ya kujikita kwenye soka moja kwa moja.
    Alianzia Sanjo FC ya Kisesa, kabla ya kwenda Scud ya Magu, baadaye Pamba FC ya Mwanza mjini, Small Boys ya Igoma, Mundu ya Zanzibar ambako alidumu kwa wiki mbili kabla ya kusajiliwa Toto African ya Mwanza mjini pia mwaka 2007. 
    Alidumu Toto hadi mwaka 2010 alipohamia Simba SC ambako alicheza kwa miaka miwili kabla ya kuondoka baada ya kumaliza Mkataba wake na kuhamia Prisons ya Mbeya kabla ya msimu uliopita kutua Ndanda FC anayochezea hadi sasa.
    Nini kilimfanya aondoke Simba SC klabu kubwa?
    “Simba sikudumu, tatizo ni mfumo mbovu wa soka yetu, kwa sababu timu zetu hazijui kama zitamtumia vipi mchezaji baada ya kumsajili,”anasema.
    Vijana wa Mweta Sports Center wakiwa tayari kwa mechi
    Sherehe za uzinduzi rasmi wa Mweta Sports Center Januari 22, mwaka huu Kisesa



    “Kama unavyojua, soka letu viongozi ndiyo wanasajili, sasa na mwalimu naye anakuwa na maamuzi yake, ikitokea viongozi wakakusajili na kocha akakubali ni bahati yako,”anasema.
    “Na niliingia pale kipindi ambacho kuna Juma Kaseja, kwa hiyo sikupata nafasi ya kucheza mbele ya Tanzania One wa wakati huo, na nilipomaliza Mkataba nikaachwa,”anasema. 
    Akiwa anaendelea kudakia Ndanda FC, Mweta anasema mipango yake ni kusimamia kituo chake ili kuhakikisha kinakuwa na shule yake rasmi, kuwawezesha vijana kupata na elimu pia.
    Mweta ni mume wa Clementina Method, ambaye wamefanikiwa kupata naye watoto wawili, wote wa kiume, William (8) na Wilson (4).
    Willy Mweta ni mdogo wa mwanamuziki maarufu nchini, Dudu Baya
    Mweta akiidakia Ndanda FC dhidi ya Yanga SC msimu uliopita katika Ligi Kuu 



    Baba yake Mweta, William Ngelela alifariki dunia mwaka 2006 wakati mama yake, Tatu Athumani yupo nyumbani Kisesa.
    Mweta ni mdogo wa mwanamuziki maarufu, Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’. “Dudu Baya ni kaka yangu ninayemfuata kuzaliwa,”anasema.‬‬‬‬
    Kipa huyo mwenye umbo kubwa, anaomba wahisani na wafadhili wajitokeze kupiga jeki kituo chake ili atimize ndoto ya kuwa na kituo kikubwa chenye hadhi, kizalishe vipaji vya wanasoka wa kisasa, wenye vipaji na elimu ya darasani.
    Dudu Baya aliwika kwenye muziki wa Bongo Fleva mwanzoni mwa muongo huu
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWETA: KIPA WA SIMBA, MDOGO WA DUDU BAYA ALIYEANZISHA ‘AKADEMI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top