• HABARI MPYA

    Wednesday, November 18, 2015

    SABABU HASWA ZA KIPIGO CHA TAIFA STARS JANA BLIDA

    Na Mahmoud Zubeiry, ISTANBUL
    MARA tu baada ya sare ya 2-2 na wenyeji Tanzania, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wachezaji wa Algeria walielekea kwenye hoteli ya Hyatt Regency (Kilimanjaro Kempinsky) kwa ajili ya mapumziko mafupi.
    Baada ya mapumziko yao ya takriban saa mbili, walioga na kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam ambako ndege yao waliyokuja nayo ilikuwa inawasubiri wao tu.
    Wakapanda ndege hiyo na kwenda moja kwa moja nyumbani, Algiers ambako walifika siku hiyo baada ya saa sita za angani.
    Na baada ya kufika Algiers, siku ilifyofuata wakaanza mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao wakati huo huo, wachezaji watatu ambao hawakuwepo katika mchezo wa kwanza wakaitwa kutoka Ulaya kuja kuongeza nguvu.
    Hao ni Mwanasoka Bora Afrika wa BBC mwaka jana, Yacine Brahimi, Belkaroui Hichem na Boudebouz Ryad, ambao wote walifika Jumapili jioni na Jumatatu walifanya mazoezi na wenzao.
    Mbwana Samatta akimuacha chini beki wa Algeria mjini Algiers

    VIPI TAIFA STARS?
    Kwa upande wa Taifa Stars, mara tu baada ya mchezo wa kwanza walikuwa wana kikao kifupi na Makamu wa Rais Dk. Samia Hassan Suluhu pale Uwanja wa Taifa.
    Baada ya hapo, wakarejea kambini kwao, hoteli ya Serena ambako baadaye tena wakawa na kikao na Kamati ya Taifa Stars, iliyowaahidi Sh. Milioni 500 iwapo wangeitoa Algeria.
    Kamati ya Taifa Stars iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Mecky Sadick waliwaweka mezani wachezaji kwa zaidi ya lisaa limoja na nusu wakifanya nao mazungumzo baada ya chakula cha usiku.
    Kutoka hapo, wachezaji wakaenda kulala saa mbili tu kabla ya kuamshwa kwa safari ya JNIA kusubiri ndege ya shirika la Uturuki, waende Algiers kupitia Istanbul.
    Wachezaji walikaa JNIA kwa saa mbili wakisubiri kuingia kwenye ndege ya Uturuki na kusafiri kwa saa nane kasoro kidogo hadi Istanbul, ambako walikaa kwa saa mbili kabla ya kuunganisha ndege kwenda Algiers ambako walitumia saa tatu.
    Msafara wa Taifa Stars ulifika Algiers saa 12 jioni za huko sawa na saa mbili usiku kwa saa za nyumbani- yaani baada ya kucha na kutwa za safari.
    Kutoka hapo, wakasafiri kwa basi kwa zaidi ya saa moja kwenda mjini Blida ambako baada ya kufika hawakupata muda wa mazoezi siku hiyo yote ya Jumapili.
    Siku iliyofuata ya Jumatatu, kutokana na uchovu wa safari, wachezaji walishinda hotelini tu kabla ya kwenda kufanya mazoezi kidogo tu kwa saa moja usiku wake Uwanja wa Mustapha Tchaker.
    Jumanne asubuhi makocha Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake, Hemed Morocco waliongozana na wachezaji wao kufanya matembezi ya nusu saa kwenye mitaa ya jirani na hoteli yao mjini Blida.
    Baada ya hapo, wakarudi kupata kifungua kinywa, baadaye chakula cha mchana na cha jioni pamoja na kupumzika kabla ya kwenda uwanjani kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
    Ni mchezo wa ugenini ambao Taifa Stars ilihitaji ushindi ili kuingia hatua ya mwisho ya mchujo wa Kombe la Dunia dhidi ya Algeria ambayo inatuacha mbali kwa kila kitu kiuwezo na uwekezaji kwenye soka.
    Baada ya dakika 45 tu, tayari Stars ilikuwa imekwishapigwa mabao matatu na kipindi cha pili wakaongezwa manne na kulala kwa 7-0, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 9-2.
    Ghoulam Faouzi wa Algeria akiwatoka wachezaji wa Tanzania

    TUMEKOSEA WAPI?
    Ni kweli Algeria wanatuzidi uwezo, tena sana, lakini bado matumaini ya kupata matokeo mazuri ugenini yalikuwapo, iwapo wachezaji wasingechoshwa baada ya mchezo wa kwanza.
    Ukifuatilia ratiba ya Stars baada ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam ukalinganisha na ya Algeria baada ya mchezo huo – kuelekea mchezo wa marudiano, huwezi kustaajabu sana timu yetu ilicheza kichovu na kufungwa magoli mengi.
    Kabla ya kuanza kufikiria sababu nyingine zote, kuhujumiwa au fitina za wenyeji, ukirudi kwenye ratiba ya timu baada ya mchezo wa kwanza kuelekea mcheo mwingine, unagundua mchawi wa kwanza ni wahusika wa timu. 
    Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wale wa Kamati ya Taifa Stars kwa kuipitisha timu safari ndefu kwenda Algiers kupitia Uturuki na vikao vingi vilivyowanyima wachezaji japo muda wa kuutathmini mchezo wa kwanza.
    Ni wazi wachezaji wa Taifa Stars walifika Algiers wakiwa wamechoka mwili na akili na hawakuwa tayari kuhimili mchezo mwingine mgumu kuliko ule wa Dar es Salaam.
    Haya ni mambo ambayo wakati tunajadili marefa na fitina za wenyeji, lazima yajadiliwe pia ikiwa tunataka kufanya vizuri katika mashindano mengine.
    Algeria wanaongeza silaha za vita, sisi tunazichosha silaha zetu kuelekea vitani.
    Kama Waalgeria walitufanyia figisu kuelekea mchezo wa marudiano, basi hazikuwa na madhara makubwa kuliko fitina tulizojifanyia wenyewe.
    Mpango wa awali ulikuwa Taifa Stars isafiri na ndege ya kukodi ya Fats Jet kwenda Algiers, ikawaje tena timu ikatumia ndege ya Uturuki?
    Ndege ya kukodi siyo tu ingepunguza muda wa safari angani – bali pia ingetufanya tujipangie wenyewe ratiba yetu ya kuondoka.
    Kuwanyima wachezaji muda wa kupumzika na kuutathmini mchezo wa awali, ilikuwa ni fitina nyingine mbaya ambayo tulijifanyia wenyewe pale Dar es Salaam.
    Kwa sasa tuseme yote. Wanatuzidi uwezo. wametufanyia fitina. Lakini fitina mbaya tulijifanyia wenyewe baada ya mchezo wa kwanza, kuelekea mchezo wa marudiano Algiers. Inauma sana, lakini ndiyo hali halisi na hapa unaweza kuwabaini watu wa kuwahusisha na matokeo haya mabaya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SABABU HASWA ZA KIPIGO CHA TAIFA STARS JANA BLIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top