• HABARI MPYA

    Friday, July 11, 2014

    MAJANGILI WAMFANYA KITU MBAYA MCHEZAJI WA ZAMANI YANGA SC

    Na Dina Ismail, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa zamani wa Yanga SC, Ally Mayay Tembele amekumbwa na janga la aina yake- ambalo limemsikitisha na kumuhuzunisha ile mbaya.
    Janga gani hilo? Akaunti yake ya barua pepe imeingiliwa na majangili ambao sasa wameanza kuwasiliana na watu wakijifanya ndiye yeye.
    Kiungo huyo aliyekuwa anaweza kucheza na nafasi za ulinzi enzi zake mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka 2000, ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba majangili hao wamekwishaanza kuwasiliana na watu wakijifanya ni yeye.
    Ally Mayay kushoto amomba marafiki zake wasiamini taarifa kwamba ana matatizo anahitaji msaada kwa sasa, kwa sababu akaunti yake ya barua pepe imeingiliwa na majangili

    “Mbaya zaidi wanasema eti mimi nimepata matatizo nahitaji msaada wa hela nyingi kujikomboa, sasa bahati mbaya zaidi, katika akaunti yangu hiyo nilikuwa nimeweka hadi nakala za pasipoti yangu na hati zangu nyingine muhimu.
    Kwa hiyo wao wanazitumia hizo pia ili kuwahakikishia watu kwamba ni mimi kweli ambaye ninaomba msaada,”amesema Mayay.
    Mchezaji huyo ambaye kwa uhodari wake uwanjani enzi zake alipachikwa jina la utani Meja, amewaomba marafiki zake na wadau mbalimbali wapuuze taarifa zote kutoka kwenye email yake kwa sasa, hadi hapo atakapolirekebisha tatizo hilo.
    “Nipo na wataalamu wa masuala haya tunajaribu kulishughulikia tatizo hilo, naomba sana marafiki na wadau wote wanaofikiwa na ujumbe wa kwamba Mayay ana matatizo na anaomba msaada kwa sasa wapuuze,”amesema.
    Mayay kulia akiwa na Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'

    Baada ya kustafu soka, pamoja na kuwa mtumishi wa Serikali, Mayay pia ni mchambuzi wa soka kwenye magazeti, Redio na Televisheni nchini kwa sasa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAJANGILI WAMFANYA KITU MBAYA MCHEZAJI WA ZAMANI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top