• HABARI MPYA

    Wednesday, June 13, 2012

    SUALA LA YONDAN HATA SI LA KUUMIZA KICHWA


    Na Mahmoud Zubeiry

    JANA, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga alisema kwamba katika sakata la beki wa kimataifa wa Tanzania, Kelvin Patrick Yondan kudaiwa kusaini mara mbili, lazima kuna klabu moja imefanya uhuni, maana yake anamtetea beki huyo kwamba hajasaini mara mbili.
    Tenga alisema hayo, wakati akijibu swali aliloulizwa kwenye Mkutano wake na Waandishi wa Habari jana, ofisi za TFF, Ilala mjini Dar es Salaam, Tenga alisema kwamba kulingana na mfumo wa sasa wa usajili kupitia mtandao, shirikisho lake halihusiki kabisa na usajili na kwamba hilo ni suala la mchezaji na klabu.
    Tenga alisema anaamini klabu hizo zitamalizana zenyewe kuhusu mchezaji huyo na akasema suala la Yondan kudaiwa kutoroshwa kambini, Taifa Stars ili akasaini Yanga halina mantiki kwa sababu mchezaji huyo ni mtu mzima ana akili zake timamu, ila kinachoendelea kwa sasa ni kelele za kinazi.
    Wiki iliyopita, beki Yondan aliibuka anasaini Yanga, kabla ya klabu yake, Simba aliyoichezea tangu mwaka 2006 kudai bado ina mkataba naye na wapinzani wao hao wa jadi, wamefanya uhuni kuzungumza naye na kumsajili wakijua hajamaliza mkataba na klabu yake.
    Lakini Yondan mwenyewe alikana kusaini Simba na kusistiza amesaini Yanga tu, waliompa Sh. Milioni 30 kwa mkataba wa miaka miwili.   
    Suala la Yondan limeteka hisia za vyombo vingi vya habari nchini tangu wiki iliyopita.
    Mapema wiki iliyopita, BIN ZUBEIRY ilikuwa chombo cha kwanza cha habari kuufichua mkataba aliosaini Yondana na Yanga na baada ya kuchapishwa magazetini, Simba SC wakaibuka na kusistiza, mchezaji huyo ana mkataba na klabu yao.
    Yondan kulia akimdhibiti Didier Drogba
    Pia, wakasema Yanga ilikiuka kanuni za usajili kumsajili mchezaji ambaye bado walikuwa wana mkataba naye na wametishia kuwashitaki FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) wapinzani wao hao.
    Lakini awali, Yondan alikaririwa na blog moja (siyo BIN ZUBEIRY) Aprili mwaka huu akisema hajasaini Yanga bali amesaini Simba. Lakini uchunguzi uliofanywa na BIN ZUBEIRY ikiwemo kuzungumza na mchezaji mwenyewe ni kwamba, aliposaini Yanga alipewa fedha nusu na sababu ya kuwakana ni kuhisi kama hatamaliziwa fedha zake.
    Kutokana na hatari ya Yondan kuwageuka, Yanga wakafanya jitihada za haraka za kummalizia fedha zake Yondan na kumpiga picha akisaini risiti za malipo yake akiwa ana fedha zake mezani na kukabidhiwa jezi ya mazoezi.
    BIN ZUBEIRY ilikuwa chombo pekee cha habari kupata picha za Yondan akisaini risiti hizo na kukabidhiwa fedha zake, kabla ya kuvunja kwenye blogs nyingine na magazeti nchini.
    Kwa Yondan kuonekana akisaini risiti hizo, ikawaumiza zaidi Simba na kutoa tamko rasmi la kulaani kitendo cha wapinzani wao hao wa jadi na kusema wanapeleka mashitaka FIFA.
    Wiki iliyopita Simba waliwasilisha malalamiko yao TFF na Tenga akawaahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo- kwa kuanzia kutaka kujua kama kweli Yondan aliondoka kambini Taifa Stars kwenda kusaini Yanga kwa kutoroka kambini au ruhusa.
    Tenga amewaahidi Simba, ikibainika Yondan alitoroka kambini hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa wahusika wote- ingawa maelezo yake ya jana yanaleta picha tofauti.
    Suala la Yondan sasa limekuwa mjadala katika vyombo vya habari nchini- na tayari hisia za kishabiki katika makala za uchambuzi wa suala hili zimekwishaanza kujitokeza. Wengi wamekwishaanza kuihukumu Yanga kwamba imefanya makosa kwa kumsajili Yondan akiwa ana mkataba na Simba.
    Kwa uzoefu wangu juu ya masuala kama hili la Yondan- sidhani kama ipo haja ya kuuhukumu upande wowote kwa sasa, iwe mchezaji au klabu zenyewe kwa sababu ndio kwanza linaibuka na litakapofika mikononi mwa vyombo husika naamini mbivu na mbichi zitajulikana.
    Yamekwishatokea masuala ya kuumiza kichwa kuhusu mchezaji kusaini mara mbili- tena wakati huo bado hakuna kanuni madhubuti, lakini yakapatiwa ufumbuzi, sembuse hili la Yondan linalokuja wakati ambao kanuni za usajili zimekaa vizuri kabisa.
    Hata kama Yondan atakuwa ana mapenzi na Yanga kiasi gani, ikibainika kweli alikwenda kusaini Yanga wakati bado ana makataba na Simba, itamgharimu yeye kwanza na Yanga wenyewe.
    Nasema kama, kwa sababu namuheshimu Yondan na naheshimu maelezo yake, akiwa mchezaji mwenye akili zake timamu alisema hajasaini Simba, amesaini Yanga. Na ninasema kama, pia kwa sababu hizo hizo za kumhesimu mchezaji huyo na maelezo yake, kwa sababu awali alisema hajasaini Yanga, ameongeza mkataba na klabu yake Simba.
    Yondan anasaini Yanga, akishuhudiwa na mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo, Seif Ahmad 'Magari'
    Kuwaita Yanga wahuni kwa sasa ni kuwaonea, kwa sababu hata TFF imetoa kumbukumbu za hadhi za mchezaji huyo na kusema, mkataba wake na Simba walionao wao uliisha Mei mwaka huu.
    Na ikumbukwe suala la Yondan na Yanga si la jana wala juzi- mchezaji huyo kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na klabu hiyo ya Jangwani na hata kwenye klabu yake amekuwa haaminiki wakati mwingine, akidaiwa yeye ni mnazi wa wapinzani na amekuwa akiwafungisha mabao katika mechi dhidi ya wapinzani wao.
    Mashabiki wenyewe wa Simba wamekuwa hawamkubali mchezaji huyo linapokuja suala la Yanga- kama ilivyokuwa kwa kiungo na Nahodha wao wa zamani, Henry Joseph Shindika, ambaye kwa sasa anacheza Norway.
    Lakini pia Yondan kufanya mzungumzo na Yanga kwa ajili ya kuhamia huko, tangu mwaka 2008 enzi hizo klabu hiyo ikiwa chini ya kocha Msrerbia, Profesa Dusan Savo Kondic, ingawa hawakufanikiwa.
    Yanga wamekuwa wakirudi tena na tena kwa Yondan bila mafanikio. Kwa sababu hiyo, hili si suala la kushitukiza nami bado ninaamini siku moja beki huyo atacheza Yanga. Sisemi hivyo kwa sababu ya mapenzi yangu na klabu, bali narejea hukumu ambayo tayari amekwishapewa siku nyingi na mashabiki wa Simba, kwamba yeye ni Yanga na kwa kuwa wahenga walisema lisemwalo lipo, au maneno yanaumba- ndio maana ninasema hivyo.
    Nimesema ni mapema kumuhukumu Yondan, kwa sababu suala lake linakuja katika picha ya usajili wa Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka Simba kwenda Yanga mwaka 2007.
    Wakati Yanga ikimsajili Chuji, Simba nayo ilisema mchezaji huyo bado ana mkataba na klabu yao- lakini mwisho wa siku kijana alicheza Jangwani.
    Watu wanawasilisha hisia zao za hasira katika hili- wakisema kwamba Yanga imefanya uhuni, lakini wamesahau tabia za wachezaji wa nchi hii? Unapofika wakati wa usajili wenyewe huhaha huku na kule, bila kuzingatia wana mikataba na klabu au la.
    Pius Kisambale baada ya kukosa kabisa timu mwaka 2009, aliwahi kunifuata kuniomba nimsaidie kupata timu, nikaenda kumuombea kwa Jamal Bayser wamsajili Mtibwa Sugar- lakini kumbe wakati huo huo alikuwa ana makubaliano na wakala mmoja ampeleleke India.
    Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage
    akionyesha mikataba yaoa na Yondan
    Alisaini Mtibwa, akachukua fedha na akatimkia India- hadi leo mimi naogopa kuwaambia Mtibwa kuna mchezaji nataka niwaletee, kwa kitendo alichofanya Pius. Nashukuru tu baadaye mchezaji huyo alirejea na kujiunga na timu hiyo.
    Victor Costa alisaini Yanga akitokea Simba, akavaa jezi kwenye Kombe lsa Mapinduzi Zanzibar, aliporejea Dar es Salaam akaenda kwenye mazoezi ya Simba Kurasini, mwaka 2005. Amri Said alisaini Yanga mwaka 2001, lakini pamoja na kupewa fedha, akabaki Simba.
    Ephraim Makoye Mahala alisaini Simba mwaka 2000, kwenye ofisi za New Habari Media Group, wakati huo zikiitwa Habari Corporations Limited kwa dili lililosukwa na mwandishi mmoja wa kike shabiki wa kufa wa Simba, lakini akabaki Yanga- ingawa baadaye alicheza Simba.
    Sioni sababu ya kuhamaki katika suala hili- haswa kwa Waandishi wa Habari, bali wanatakiwa kwanza kujiridhisha na ukweli ndipo watoe hukumu.
    Yondan huyu mmoja alisema hajasaini Yanga amesaini Simba, akasema tena hajasaini Simba amesaini Yanga. Kwa nini sasa tuhamaki na kuendesha magari kwa visirani na hasira mwishoni tufanye ajali barabarani bure?
    Ipo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ipo Kamati ya Nidhamu ya TFF, kutoka kwao tunatarajia watalipatia ufumbuzi suala la Yondan. Baada ya hapo, tutakuwa na fursa nzuri ya kufungua mijadala mipya. Nawasilisha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SUALA LA YONDAN HATA SI LA KUUMIZA KICHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top