• HABARI MPYA

    Monday, June 25, 2012

    DIRA YA DOGO ASLAY ILIVYO TOFAUTI NA WENGINE


    Na Herieth Makwetta
    WAKATI masomo yakimshinda msanii Dogo Janja, msanii mwenzie mwenye umri mdogo na anayefanya vizuri kwenye muziki wa Bongo, Dogo Aslay, amejikita kwenye elimu huku akijenga mjengo wa heshima kwa familia yake jijini Dar es Salaam.

    Msanii huyo anayetamba na wimbo wa 'Naenda Kusema' ameithibitishia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam kuwa kwake elimu ni kitu cha kwanza na wala hazuzuki na vitu vya thamani kama simu aina ya Blackberry anayomiliki.

    Aslay ameweka bayana kwamba anaendelea na ujenzi wa nyumba kubwa ya familia yake maeneo ya Mbagala nje kidogo ya Dar huku yeye akiishi kwenye kituo cha kukuza vipaji cha 'Mkubwa na Wanawe' chenye makazi ya wasanii chipukizi wa muziki na studio.

    Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Temeke anayetarajia kuzindua albamu na kitabu cha maisha yake na filamu Juni 24, anasema umri mdogo pamoja na kumiliki simu ya gharama hakumzuii kufanya vizuri darasani.

    "Sioni kama simu inanikwamisha, kwani ninakaa na simu kwa masaa machache sana kabla sijaanza kushughulika na masomo. Ninaipa nafasi katika maisha yangu, na sio kwamba nakaa nayo muda wote," anaeleza Aslay ambaye hata hivyo ameweka wazi kuwa anapokuwa shule huwa hatembei na simu hiyo.

    "Tuna michezo shuleni, ninacheza vizuri sana mpira, na pia ni mwimbaji mzuri, lakini walimu wangu wananiona nina kipaji cha uongozi, lakini mimi sihitaji kuwa kiongozi.

    "Nikijitwisha uongozi nahisi nitakuwa tayari nimebeba majukumu mengi, mimi bado nina umri mdogo, nasoma na muziki nao unaningoja."

    Akielezea ratiba yake ya siku msanii huyu ambaye hivi sasa anatamba na kibao kipya cha 'Umbea Umbea' alichomshirikisha Chege anasema: "Meneja wangu Fela amenipangia ratiba, kwa kuwa darasani naingia mchana hivyo muda wa asubuhi ni kujisomea na kufanya mazoezi ya shule.
    "Mchana nakwenda shule, nikitoka darasani napitia twisheni.

    Nikirudi nyumbani jioni ndiyo nafanya mazoezi ya muziki. Huwa naingia studio saa moja usiku hadi saa mbili, kisha nakwenda kulala. Hiyo ndiyo ratiba yangu ya siku.

    "Ninamalizia kujenga nyumba ya familia yenye vyumba zaidi ya vitatu na pia nimemwongezea mama yangu mtaji, ambao nilimpa mwaka jana. Ni mtaji wa biashara yake ya vitenge.

    "Kwa ujumla nafurahi, ingawa siishi na familia, lakini nikienda kuwatembelea naona sasa familia yangu inaishi maisha ya furaha."
    Anasema anaipenda familia yake kwani ilimpa sapoti kubwa mpaka kuweza kufikia alipo.

    "Wazazi walinipa sapoti na hivi sasa nasomeshwa na kituo na pia kazi zangu nasimamiwa na kituo, lakini najitahidi kuhakikisha wazazi wangu wanapata kile walichokipanda kwangu na situmii pesa ovyo," anasema.

    "Fedha zangu napenda ziwe mikononi mwa wazazi, kwani najua nitaharibikiwa iwapo nitashika pesa kila wakati.

    "Nikifanya shoo nikipewa pesa nawatumia wao na nikipata fedha wakati mwingine nikihitaji kufanya matumizi yangu binafsi naweza, lakini nahitaji mama yangu ajue."

    Naye Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family na Mkubwa na Wanawe, Said Fella, anasema Dogo Aslay atazindua albamu hiyo, kitabu pamoja na filamu ambapo zote amezipa jina la Naenda Kusema.

    Anasema albamu hiyo ina jumla ya nyimbo 10 ambayo ameirekodia katika studio ya Poteza Records chini ya mtayarishaji Suresh pamoja na Alow Nem.



    SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI:
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DIRA YA DOGO ASLAY ILIVYO TOFAUTI NA WENGINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top