• HABARI MPYA

    Wednesday, June 27, 2012

    YANGA KUSAJILI WACHEZAJI WAZURI SI KUWA NA TIMU NZURI


    Na Mahmoud Zubeiry

    YANGA inasifiwa kufanya usajili mzuri kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, miongoni mwa wachezaji iliyowasajili wakiwemo Kelvin Yondan, Ally Mustafa ‘Barthez’ kutoka Simba na Frank Damayo kutoka JKT Ruvu.
    Kulingana na hali halisi ya uwezo wa wachezaji hao kwa sasa, hususan Yondan, wenyewe wanamuita Vidic na Damayo, mashabiki wa Yanga wamesuuzika mno na nafsi zao. Wanaamini wachezaji hao na wengineo, wataifanya timu yao iwe tishio msimu ujao.
    Yanga sasa wana ndoto nyingi sana juu ya timu na japokuwa mwakani hawatashiriki michuano ya Afrika, lakini wanaona kabisa wamekwishatetea Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
    Yanga tayari wa ndoto za kulipa zile 5-0 walizopigwa na watani wao wa jadi, Simba msimu huu. Wanaota kurejesha ubingwa wao wa Ligi Kuu na kwa ujumla heshima yao katika soka ya Tanzania, waliyoipoteza msimu uliopita.
    Kwa ujumla wana matumaini makubwa sana, hasa wakizingatia Mwenyekiti wao atakuwa Yussuf Manji, Makamu wao Mwenyekiti Clement Sanga na Wajumbe kama Abdallah Bin Kleb, Peter Haule na wengineo- wana Yanga, wana matumaini makubwa sana na kikosi chao kipya.
    Lakini pamoja na ukweli huo, kuna mambo ambayo wana Yanga wanatakiwa wayatambue, kubwa ni kwamba; Kusajili wachezaji wazuri ni suala moja na kuwa na timu nzuri ni suala lingine.
    Yanga wamefanikiwa mtihani wa kusajili wachezaji wazuri, na sasa wanatakiwa wapitiE katika zoezi gumu zaidi la kutengeneza timu nzuri ya ushindani kwa mashindano ya ndani na nje.
    Bahati nzuri, Yanga wana muda wa kutosha kwa sababu msimu wote ujao utakuwa wa kutengeneza tu timu yao kwa kuwa hawashiriki michuano ya Afrika- hivyo kama watafanikiwa kufuzu na mtihani huo pia, tegemea kabisa Yanga ya 2014 itakuwa tishio hadi Afrika.
    Lakini hiyo timu nzuri inatengenezwaje? Kwanza kuwa na mwalimu bora, atakayepeta fursa na wasaa mzuri na wa kutosha wa kuwaandaa wachezaji. Haitoshi tu kusajili wachezaji wazuri na kisha unawakabidhi kwa msimamizi wa mazoezi, ni hatari kwa vipaji vyao.
    Yondan mazoezini Yanga
    Yanga wanatakiwa kutengeneza sera nzuri za benchi la ufundi, ambalo litakuwa na nguvu na kuheshimiwa na wachezaji, tofauti na ilivyo hivi sasa, mchezaji anamuheshimu Seif Magari, anamdharau Freddy Felix Minziro.
    Yanga inatakiwa kuwa wazi kwa wachezaji wake, kuwaambia imewasajili kwa ajili ya kufanya kazi na wasilewe sifa na kuanza kupandisha mabega juu, uwanjani hawajitumi, matokeo yake wanarudi kule kule, kwenye kununua mechi.
    Haiwezekani, usajili huu wa Yanga naomba niseme mapema ulikuwa makini mno, tofauti na usajili wa miaka miwili, mitatu iliyopita na timu iliyopewa jukumu hilo, ililifanikisha kwa umakini wa hali ya juu.
    Kwa sababu hiyo basi, wachezaji lazima wacheze soka uwanjani, watengeneze matokeo mazuri kwa uwezo wao. Wadumishe viwango vyao, ili waendelee kuwapo timu ya taifa. Lakini kubwa na la msingi ni mashabiki wa Yanga kuwa na subira kabla ya kupata timu nzuri.
    Yanga watawaona wachezaji wao wazuri katika Kombe la Kagame na watafanya sana vitu adimu binafsi na ikibidi, kweli watatetea hadi Kombe lao- lakini kuwa na timu nzuri kwa maana ya timu inayocheza soka ya kuelewana, iliyotokana na mafundisho, wana Yanga wanatakiwa kuwa na subira.
    Kama watapata mwalimu mzuri, naamini akipata fursa na wasaa mzuri na wa kutosha, kuanzia mzunguko wa pili Yanga itakuwa inacheza ‘kitenisi’ cha kutisha- ila kama ubabaishaji utaendelea na hakutakuwa na sera nzuri za benchi la ufundi, mafunzo, nidhamu na kujali maslahi ya wachezaji, basi wachezaji hawa Desemba tu wataonekana hawafai. Alamsiki!
    Wachezaji wa Yanga mazoezini, Jerry Tegete kushoto na Godfrey Taita

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KUSAJILI WACHEZAJI WAZURI SI KUWA NA TIMU NZURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top