• HABARI MPYA

    Monday, June 25, 2012

    PETER SHILTON: Aliyefungwa bao la ‘Mkono wa Mungu’ na Maradona


    Shilton alivyo sasa

    PETER Shilton ni mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa ya England aliyezaliwa Septemba 18, mwaka 1949 Mjini Leicester, England.
    Anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi katika timu ya taifa ya England, zaidi ya wachezaji wengine, amecheza jumla ya mechi 125.
    Katika miaka 30 aliyocheza soka, ameweza kucheza klabu tofauti 11, pamoja na fainali tatu za Kombe la Dunia na michuano miwili ya Mataifa ya Ulaya na zaidi ya mechi 1,000 za michuano.
    Shilton hakucheza fainali za Kombe la Dunia hadi alipofika umri wa miaka 32, lakini amecheza jumla ya mechi 17 na kuweka rekodi ya kutofungwa mechi 10 katika fainali hizo za Kombe la Dunia, rekodi ambayo pia imewekwa na mlinda mlango wa Ufaransa, Fabien Barthez.
    Alipokuwa Nottingham Forest alishinda mataji mawili ya UEFA Super Cup, ubingwa Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Ligi na mataji mengine mengi.
    Shilton alikuwa ni mwanafunzi wa umri wa miaka 13 katika shule ya King Richard III Boys School, iliyopo Leicester, wakati alipoanza kufanya mazoezi na klabu ya Leicester City mwaka 1963.
    Mei mwaka 1966, akiwa na umri wa miaka 16, Shilton alianza kucheza kwa mara ya kwanza katika klabu ya Leicester dhidi ya Everton, kuanzia hapo alikuwa akipangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
    Pamoja na kuwa na msimu mbaya wakiwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini walifanikiwa kuingia fainali ya Kombe iliyochezwa Wembley, akiwa na umri wa mika 19. Shilton alikuwa ni mchezaji mdogo katika mechi hiyo, lakini walifungwa kwa bao 1-0 na Manchester City.
    Timu yake ilishuka daraja, lakini aliamua kubaki nayo, pamoja na kucheza timu ya daraja la chini, lakini alimshawishi kocha wa timu ya taifa ya England wakati huo, Alf Ramsey, kumpa nafasi ambapo alicheza dhidi ya Ujerumani Mashariki Novemba mwaka 1970. England ilishinda mabao 3–1.
    Baadaye aliisaidia Leicester kupanda daraja na kupata nafasi nyingine ya kuichezea timu ya taifa katika mchezo uliomalizika bila ya kufungana dhidi ya Wales katika Uwanja wa Wembley.
    Na mechi yake ya tatu, huku ikiwa ni ya kwanza ya ushindani alicheza dhidi ya Uswisi, ambapo walitoka sare 1–1, katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Ulaya.
    Aliendelea kuichezea England mechi ya nne na ya tano, wakati huo Shilton akiwa mlinda mlango namba mbili na Oktoba mwaka 1972, mlinda mlango namba moja Gordon Banks, alipata ajali na kupoteza uwezo wa kuona na kukatiza soka lake, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Ray Clemence wa  Liverpool.
    Shilton aliondoka Leicester na kujiunga na Stoke City kwa ada ya pauni 325,000, wakati huo wakiendelea kugombea namba kwenye kikosi cha England na Clemence, ambaye alionekana kumzidi Shilton kwa kucheza mechi nane kati ya tisa.
    Shilton alicheza mara moja tu mwaka 1975 kwenye kikosi cha England, hakucheza kabisa mwaka 1976 na 1977 alicheza mara mbili.
    Msimu wa mwaka 1976 Manchester United walimtaka Shilton na Stoke walikubali kumtoa kwa pauni 275,000, lakini walishindwa juu ya mshahara alioutaka kipa huyo na kuamua kuachana naye.
    Shilton enzi zake
    Aliendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Stoke, ingawa kilishuka daraja mwaka 1977, Nottingham Forest walitoa ofa ya pauni 250,000 na Shilton alikubali kusaini msimu mpya na timu hiyo ya Forest kupanda daraja.
    Walishinda Kombe la Ligi katika mchezo wa marudiano baada ya kutoka sare dhidi ya Liverpool, katika mchezo ambao Shilton alionyesha uwezo wake, akiokoa michomo na vichwa vya Mick Ferguson. Shilton alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya PFA, kocha mpya wa England, Ron Greenwood, alimchagua Shilton na kumuacha Clemence na mashabiki na wachambuzi wengi wa soka kukosoa jambo hilo.
    Shilton, alisaidia England kwa ajili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1980 nchini Italia, ushindi dhidi ya Hispania, ulimfanya ashinde mechi 30.
    Mlinda mlango huyo, aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kupigwa faini ya pauni 350, huku tetesi za kutaka kuondoka Nottingham mwaka 1982, zilianza kuzagaa.
    Shilton, aliondoka Forest na pamoja na kutakiwa na Arsenal, alikwenda kucheza Southampton na kukutana na wachezaji wenzake wa timu ya taifa kwenye klabu hiyo kama vile, Kevin Keegan, Alan Ball na Bobby Robson, aliivunja rekodi ya Bank kwa kucheza mechi 188, wakati mwenzake alicheza 73.
    Wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986, England walianza taratibu kwa kupoteza mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya Ureno, wakatoka sare na Morocco, wakati huo Robson akiwa majeruhi na Wilkins alipewa kadi nyekundu.
    Kutokana na kukosekana kwao wote, Shilton alipata nafasi ya kucheza mechi na kuwa nahodha wa England na kuichapa Poland 3–0 kwenye mechi ya mwisho ya kundi lao, mabao yote yakifungwa na Gary Lineker.
    Walikutana na Paraguay katika hatua iliyofuata na Shilton kufanya kazi kubwa ya kuokoa mipira ya hatari katika kipindi cha kwanza, England walishinda 3-0 mabao yakifungwa na Lineker mawili na moja Peter Beardsley.
    Hatua ya robo fainali walikutana na Argentina, mechi iliyoonyesha uwezo wa Shilton katika kipindi chake chote cha soka.
    Nahodha wa Argentina, Diego Maradona, alikuwa nyota wa michuano hiyo, lakini katika mchezo wao, England walimudu kumbana katika kipindi cha kwanza, kazi ilikuwa pale kipindi cha pili, Maradona alipobadili uchezaji wake na kumchanganya sana Shilton.
    Maradona alianza kushambulia na kuingia kila wakati kwenye eneo la hatari England, beki wa England alifanya madudu na Maradona, akawahi mpira kwenye eneo la hatari, lakini Shilton aliokoa mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo wakiwa wamebaki wawili.
    Baadaye Maradona alitumia mbinu nyingine ya kumfunga mlinda mlango huyo baada ya kushindwa kufanya hivyo hapo mwanzo.
    Ulipigwa mpira na Maradona akaruka na kuangalia ule mpira wakati Shilton akiunyemelea hewani, Maradona alinyoosha mkono wake na kuugonga mpira na ukaingia nyavuni.
    Wachezaji wa England pamoja na mlinda mlango wao walilalamika kwamba Maradona ameshika, lakini mwamuzi kutoka Tunisia, Ali Bin Nasser, alikubali bao hilo.
    Baadaye Maradona alipoulizwa alisema ni bao la mkono wa Mungu, na mwamuzi Nasser hakupewa nafasi nyingine tena ya kuchezesha michuano mikubwa kama hiyo.
    Hivyo Shilton, aliepuka kukosolewa kutokana na vyombo vya habari vya England kuona tukio zima lilivyokuwa.
    Lakini baadaye Maradona alifunga bao jingine la kawaida, baada ya kuwakusanya mabeki wote wa England pamoja na Shilton na kupasia nyavu zikiwa tupu. Lineker alifunga bao moja na kukaribia kusawazisha lakini bahati haikuwa yao, walitolewa katika hatua hiyo ya robo fainali.
    Shilton aliendelea kuichezea England kwenye michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1988, iliyofanyika Ujerumani Mashariki.
    Juni mwaka 1989, Shilton alivunja rekodi ya Bobby Moore, aliyecheza mechi 108, wakati yeye akicheza 109, alicheza mechi tatu bila kufungwa katika kampeni za kushiriki fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990 na wakafanikiwa kufuzu.
    Baada ya kustaafu kuichezea timu ya Taifa mwaka mwaka 1991, alikataa kuwa kocha kuchukua nafasi ya Stan Ternent kwa ajili ya kuinoa Hull City.
    Yeye na mkewe Sue, walioana mwaka 1970 na wana watoto wawili, Michael na Sam.
    Sam anacheza soka katika nafasi ya kiungo, amecheza klabu kubwa mbalimbali kama Plymouth Argyle na Coventry City.
    Desemba 18 mwaka 2011, ilitangazwa kwamba ametengana na mkewe baada ya kuishi wote miaka 40 ya ndoa yao.
    WASIFU WAKE
    JINA: Peter Leslie Shilton
    KUZALIWA: Septemba18, 1949 (62)
    ALIPOZALIWA: Leicester, England
    UREFU: Futi 6 inchi 1
    NAFASI: Mlinda mlango

    TIMU ZA VIJANA
    1963–1966 Leicester City

    TIMU ZA WAKUBWA
    1966–1974 Leicester City, (mechi 286, bao 1)
    1974–1977 Stoke City, (mechi 110)
    1977–1982 Nottingham Forest, (mechi 202)
    1982–1987 Southampton, (mechi 188)
    1987–1992 Derby County, (mechi 175)
    1992–1995 Plymouth Argyle, (mechi 34)
    1995    Wimbledon, (hakucheza)
    1995    Bolton Wanderers, (mechi 1)
    1995–1996 Coventry City, (hakucheza)
    1996    West Ham United, (hakucheza)
    1996–1997 Leyton Orient, (mechi 9)
    Jumla amecheza mechi 1,005 na bao 1
    (Tangu 1970 hadi 1990, aliichezea     England mechi 125)
    UKOCHA:  1992–1995 Plymouth Argyle
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PETER SHILTON: Aliyefungwa bao la ‘Mkono wa Mungu’ na Maradona Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top