• HABARI MPYA

    Friday, June 29, 2012

    SIMBA WAPELEKA TIMU ZANZIBAR


    Kikosi cha Simba msimu uliopita

    Na Prince Akbar
    MABINGWA wa soka Tanzania, Simba SC wamethibitisha kushirikimichuano ya Kombe la Ujirani Mwema Tanzania, iliyopangwa kuanza Jumapili wiki hii visiwani Zanzibar.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange, amesema maamuzi ya kushiriki katika mashindano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya Ufundi ya Simba.
    “Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Tanzania lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo kwa sasa,” alisema.
    Makamu alisema zaidi ya kushiriki michuano hiyo, Simba pia itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Kagame lililopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu.
    Pia, alisema Simba itatumia ziara hiyo kupeleka kombe la Ligi Kuu ya Vodacom kwa wana Simba wa Zanzibar ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa Vodacom na pia.
    “Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0, Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar,” alisema Kaburu.
    Simba itaanza michuano hiyo siku ya Jumatatu ambapo itacheza na Mafunzo ya Zanzibar katika pambano lililopangwa kufanyika usiku. Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni lakini imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.
    Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo ambapo Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Simba, Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).
    Wakati huo huo: Mabingwa hao wa Tanzania, Simba SC, wanatarajiwa kucheza na mabingwa wa soka wa Uganda, Express FC, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, maandalizi yote kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika na kwamba kikosi cha Simba kitaundwa na wachezaji wapya na wa zamani.
    Huu utakuwa mchezo wa pili baina ya timu hizo, katika ziara hii ya Tae Wekundu wa Kampala, baada ya awali kutoka sare ya 1-1 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAPELEKA TIMU ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top