• HABARI MPYA

    Tuesday, May 05, 2020

    TFF YAZIKUMBUSHA KLABU NCHINI KUTOANZA MAZOEZI HADI SERIKALI ITAKAPOTOA TAMKO RASMI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa tahadhari kwa timu kutoanza mazoezi ya pamoja hadi hapo tamko la Serikali litakapotolewa – ingawa imesema bado inaendelea na mchakato wa kurejesha Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Pombe Joseph Magufuli.
    Lakini TFF imesema kwamba mchakato huo bado ni wa ndani, hivyo wanachama wake wote wanapaswa kuendelea kutekeleza agizo la awali la Serikali la kuepuka mkusanyiko kwa maana ya kutoanza maozezi ya pamoja hadi hapo maelekezo mengine yatakapotolewa.
    Juzi Rais Magufuli wakati anamuapisha Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba wilayani Chato mkoani Geita alisema kwamba anafikiria kuruhusu Ligi Kuu iendelee kwa sababu hajasikia mwanamichezo hata mmoja ameathiriwa na virusi vya corona.

    Na jana Bodi ya Ligi (TPLB) ilikuwa ina kikao na Kamati ya Tiba ya TFF kupata ushauri wa kitaalamu juu ya namna Ligi itakavyoendeshwa kwa kuzingatia tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.
    Kamati ya Tiba ipo chini ya Mwenyekiti, Dk. Paul Marealle, Makamu wake, Dk. Fred Limbanga na Wajumbe Dk. Norman Sabuni, Dk. Lisobina Kisongo, Dk. Eliezer Ndama, Dk. Billy Haonga, na Dk. Violet Lupondo. 
    Lakini leo TFF imesema; “Pamoja na michakato ya ndani ya TFF na TPLB kuhusu mashindano yake kuendelea, bado hatima ya kurudi kwa mashindano yote itategemea uamuzi wa Serikali, ambayo itaelekeza muda mwafaka wa kurejea kwa mashindano,”.
    Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.
    Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAZIKUMBUSHA KLABU NCHINI KUTOANZA MAZOEZI HADI SERIKALI ITAKAPOTOA TAMKO RASMI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top