• HABARI MPYA

    Wednesday, May 27, 2020

    KOCHA MRUNDI KUANZA KUINOA AZAM FC KUJIANDAA KUMALIZIA MSIMU WA LIGI KUU

    Na Mwandshi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Mrundi Bahati Vivier, tayari yupo nchini kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo, inayoanza mazoezi rasmi leo Jumatano, kwa ajili ya kumalizia mechi zilizobakia za msimu huu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
    Vivier ambaye atakuwa sambamba na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, anaanza kukinoa kikosi hicho akisubiria kurejea nchini kwa Kocha Mkuu, Aristica Cioaba na Kocha wa Viungo, Costel Birsan, waliokwama nchini kwao, Romania.
    Makocha hao wanasubiria kurejea kwa usafiri wa ndege katika anga la Ulaya mwezi ujao, kufuatia makampuni mengi ya usafiri wa anga kusimamisha shughuli zao baada ya mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19). 

    Mrundi Bahati Vivier anatarajiwa kuanza kuinoa Azam FC leo kujiandaa kumalizia msimu

    Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa pamoja itaendelea kuanzia Juni baada ya kusimama tangu Machi 17, mwaka huu kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    Na katika ASFC timu zilizofanikiwa kutinga Robo Fainali ni Alliance FC ya Mwanza, Namungo FC ya Ruangwa, Lindi, Ndanda FC ya Mtwara, Kagera Sugar ya Bukoba, Azam FC, Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Sahare All Stars ya Tanga, timu pekee ya Daraja la Kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MRUNDI KUANZA KUINOA AZAM FC KUJIANDAA KUMALIZIA MSIMU WA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top