• HABARI MPYA

    Saturday, May 30, 2020

    NI MZIGO MZITO CHRISTIAN BELLA ANABEBESHWA, DANSI HAILIPI TENA

    NAKUMBUKA wakati ajali ya MV Bukoba ilipotokea mwaka 1996 na kukatisha uhai wa mamia ya Watanzania, nilipata kumshuhudia mmoja wa waombolezaji ambaye aliniacha kinywa wazi.
    Muombolezaji yule aliyepoteza mtoto wake wa kiume kwenye ajali ile, alikuwa analalamika kwanini mwanaye amefariki, kwanini hakuwa mmoja kati ya watu waliosalimika, kwanini basi hawakufariki watu wote, kwanini wengine wafe halafu wengine wasalimike.
    Pamoja na kutambua kwangu kuwa mara nyingi wafiwa hushikwa na kiwewe hadi hata kumkufuru Mungu, lakini lile la mfiwa kutaka watu wote wafariki kwenye ajali liliniduwaza sana.

    Hali hii ipo pia kwenye muziki wa Dansi ambao umeyumba kidogo sokoni ambapo wale wanaoonekana kufanikiwa kuokoka kwenye anguko la soko la muziki huo, wananyooshewa kidole pamoja na kutazamwa kwa jicho la kwanini.
    Christian Bella, mwimbaji wa dansi anayetusua vizuri sokoni, amekuwa mlengwa mkuu, anakumbana na maneno makali kutoka kwa wadau na mashabiki wa muziki wa Dansi.
    Bella pengine kwa kutambua ugumu wa soko la muziki wa Dansi, ameamua kuingiza vionjo vya muziki wa Kizazi Kipya (Bongo Fleva) kwenye nyimbo zake nyingi, hatua ambayo imekuwa na afya kubwa kwake.
    Hili limekuwa likiwakera wadau wengi hali inayonikumbusha yule muombolezaji wa ajali ya MV Bukoba, ni kama vile wadau wanasikitishwa kwanini Bella anatusua huku wengine wakisuasua, ni kama vile wanataka wanamuziki wote wa Dansi wazame pamoja, asitokee wa kusalimika.
    Bella anabebeshwa mzigo mkubwa sana na wadau wa Dansi, anachukuliwa kama ndiyo mwarobaini wa kuinua Dansi, wanataka asitoke nje ya mstari, ang’ang’ane na muziki huo hata kama utamletea njaa.
    Wadau hawaoni mtu mwingine wa kumbebesha mzigo wa kulikwamua Dansi zaidi ya Bella, wala hawakumbuki kuwa mwimbaji huyu alishazama sokoni akiwa ndani ya Akudo Impact, hawakumbuki kuwa Bella alitumia juhudi zake binafsi kurejea upya sokoni, hawakumbuki kuwa hawakumsadia chochote zaidi ya kusema Bella amekwisha. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kusema jamaa anabwia ‘unga’.
    Dr Remmy aliimba muziki hauna mwenyewe. Hebu tumwache Bella afanye kazi yake kwa maslahi ya maisha yake na familia yake na kwa maslahi ya soko la muziki kwa ujumla, tusipende kuweka mipaka isiyo na tija, Bella ataendelea kuwa msanii wa Dansi.
    Suala la kuweka vionjo vya aina tofauti kwenye muziki wa Dansi halikuanza leo wala jana. Tafuta wimbo “Mambo Bado” wa Orchestra Makassy ukutane na ladha ya Pop, tafuta wimbo “Nimekusamehe Lakini Sitokusahau” wa Washirika Stars ukutane na mirindimo ya Reggae.
    Zamani baadhi ya bendi zilihakikisha kuwa zina mwimbaji maalum wa nyimbo za kizungu, hata Twanga Pepeta waliwahi kuwa na utaratibu huo. Yote hiyo ilikuwa ni moja ya njia za kupanua wigo wa biashara, hivyo tusimshangae Bella.
    Ipo tabia moja ambayo sijui dawa yake itapatikana lini – tabia ya kuwachukia wenye kujua, kuwaonea choyo na kuwaombea mabaya. Yaani mtu anakonda kwa mafanikio ya mwenzie au ananenepa kwa anguko la jirani yake! 
    Kwenye sanaa hii kitu imevuka mipaka, kuna chuki za kufa mtu na kwa mara nyingine tena napenda kumtaja mwimbaji Christian Bella kama mmoja wa watu wanaokumbana na kadhia ya tabia hiyo ya kikorosho.
    Bella anaambiwa ana roho mbaya na anaringa, lakini mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya wasanii wa Dansi na mashabiki wa muziki wa muziki huo wanatamani kumtenga – eti hapigi Dansi, anapiga Bongofleva - mada ya kijinga kabisa ambayo kama utaifuatilia kwa kina hutapata jibu la uhakika kuwa muziki wa Dansi ni upi na Bongofleva ni ipi. 
    Hoja ya kijinga zaidi kutoka kwa baadhi ya wasanii marafiki zangu wa muziki wa Dansi ambao katika vikao vyetu vya kuambukizana ujinga, ni pale wanapothubutu kusema siku Bella akitoa wimbo mbovu, ukakosa kiki maredioni, basi huo ndo utakuwa mwisho wake na itakuwa fursa kwa msanii mwingine wa Dansi kupanda juu kuchukua nafasi yake. 
    Najiuliza, hivi Bella hajawahi kutoa wimbo mbaya? Bella hajawahi kutoa wimbo uliokosa kiki? Hivi ngoma 'Acha Kabisa' aliouimba na gwiji Koffi Olomide ilikuwa nzuri? Ilipata kiki baada ya kuachiwa hewani? Je Bella mwenyewe anahangaika hata kuipiga mara kwa mara ukumbini? Ok wacha tufanye kuwa Bella hajawahi kutoa wimbo mbaya, tuendelee kusubiri nyimbo mpya mbovu kutoka kwake ili tuone atakavyoporomoka. 
    Anachokifanya Bella ni kusoma soko la muziki linahitaji nini kisha anapenya hapo hapo na iwapo wasanii wa Dansi wataendelea kukaa kitako na kumtenga basi wataishia kusema jamaa hapigi Dansi, huku mwenzao akitengeneza pesa. Bella hawezi kuwa hapo alipo kwa miaka nenda rudi, ni lazima siku moja atashuka tu.
    Ally Chocky akiwa na bendi ya Mchinga Generation aliwahi kuimba wimbo ulioitwa 'Kila Chenye Mwanzo', ukiusikiliza kwa makini wimbo ule sambamba na mifano iliyotolewa, basi utakuwa umepata elimu kubwa juu ya dhana ya ‘Kila chenye mwanzo kina mwisho.’ 
    Lakini kushuka kwake hukutakuwa sababu ya msanii mwingine kupanda juu, bali atakayepanda ni yule mwenye kazi bora inayokidhi mahitaji ya soko na ikumbukwe kuwa hili linaweza kufanyika hata bila kusubiri siku ya Bella kuporomoka. Tujaribu kuepuka dhana ya usemi wa ‘Aliye juu mngoje chini’. 
    Enzi za kufanya muziki kama wito zimepita, muziki sasa ni ajira, muziki ni maisha, ubunifu wa hali ya juu unahitajika na msanii anapaswa kubadilika kulifuata soko, bila hivyo tutaendelea kukesha tukiomba baadhi ya watu wastaafu au waporomoke kisanii ili tukarithi nafasi zao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MZIGO MZITO CHRISTIAN BELLA ANABEBESHWA, DANSI HAILIPI TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top