• HABARI MPYA

    Friday, May 29, 2020

    MECHI ZOTE ZILIZOSALIA ZA LIGI KUU TANZANIA BARA KUCHEZWA NYUMBANI NA UGENINI KUANZIA JUNI 13

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MECHI zilizosalia za Ligi Kuu ya Tanzania Bara itachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kuanzia Juni 13, mwaka huu kama kawaida tofauti na tamko la awali la Serikali kwamba itachezwa kwa vituo.
    Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amesema leo Jijini Dar es Salaam kwamba maazimio hayo waliyafikia jana kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi na kuyafikisha Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.
    Kasongo alisema ratiba nzima ya mechi zilizosalia za Ligi Kuu ya Tanzania itatolewa Jumapili ingawa hakusema kama mashabiki wataruhusiwa au la.
    Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema mechi zilizosalia za Ligi Kuu zichezwe Dar es Salaam pekee katika viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex pamoja na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) iliyofikia hatua ya robo Fainali.
    Kuhusu mechi za Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, Waziri Mwakyembe alisema kwamba zitachezwa Jijini Mwanza kwenye viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana na kwamba katika mashindano yote mashabiki hawataruhusiwa kungia uwanjani.
    Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    Na katika ASFC timu zilizofanikiwa kutinga Robo Fainali ni Alliance FC ya Mwanza, Namungo FC ya Ruangwa, Lindi, Ndanda FC ya Mtwara, Kagera Sugar ya Bukoba, Azam FC, Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Sahare All Stars ya Tanga, timu pekee ya Daraja la Kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI ZOTE ZILIZOSALIA ZA LIGI KUU TANZANIA BARA KUCHEZWA NYUMBANI NA UGENINI KUANZIA JUNI 13 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top