• HABARI MPYA

    Tuesday, May 26, 2020

    BAO AMBALO SAMATTA ALIWAFUNGA LIVERPOOL UWANJA WA ANFIELD LASHINDA TUZO KRC GENK

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAO alilofunga Mbwana Ally Samatta akiwa KRC Genk ya Ubelgji dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Novemba 5, 2019 Uwanja wa Anfield limeteuliwa kuwa Bao Bora la Msimu na klabu yake hiyo ya zamani iliyochapwa 2-1 siku hiyo.
    Ni Januari tu mwaka huu KRC Genk ilimuuza Mbwana Samatta klabu ya Aston Villa baada ya kuwa naye tangu Januari 2016 ilipomnunua TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
    Samatta aliyekuwa anacheza Anfield kwa mara ya kwanza usiku wa Novemba 5 mwaka jana, aliifungia KRC Genk bao hilo dakika ya 40 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen.
    Mbwana Samatta akiifungia KRC Genk dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Novemba 5, 2019 Uwanja wa Anfield

    Na hiyo ilifuatia mabingwa wa Ulaya, Liverpool kutangulia kwa bao la Georginio Wijnaldum dakika ya 14 akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya KRC Genk, kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain kuwafungia Wekundu wa Anfield bao la ushindi dakika ya 53 akimalizia pasi ya Mohamed Salah.
    Inaaminika ni kazi yake nzuri Anfield na kwa ujumla kiwango chake kwenye Ligi ya Mabingwa ndiyo ilimfungulia milango ya kuhamia England baada ya kusajiliwa Aston Villa kwa dau la Pauni Milioni 10 akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.
    Samatta mwenye umri wa miaka 27 sasa, aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Lubumbashi, DRC ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016.
    Samatta aliifunga Genk mabao 76 katika mechi 191 na kwa sasa ndiye Nahodha wa timu yake ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambayo ameifungia mabao 20 katika mechi 56 tangu mwaka 2011.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAO AMBALO SAMATTA ALIWAFUNGA LIVERPOOL UWANJA WA ANFIELD LASHINDA TUZO KRC GENK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top